Mabasi mapya 49 ya Udart kuingizwa barabarani

Dar es Salaam. Mabasi 49 ya usafiri wa haraka maarufu mwendokasi yaliyoingia nchini yameanza kupakuliwa bandarini, huku matarajio yakiwa kuanza kazi ndani ya mwezi huu.

Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Gabriel Katanga, amesema hayo leo Ijumaa Januari 9, 2026 alipozungumza na Mwananchi kuhusu hatua iliyofikiwa ya mabasi hayo kuingizwa nchini.

Wiki hii, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Riziki Shemdoe alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ukarabati wa mabasi yaliyoharibika alizungumzia kuhusu ujio wa mapya.

Shemdoe alisema Serikali imetoa Sh20 bilioni za ununuzi wa mabasi 100, akiitaka Udart kuhakikisha yanatolewa haraka bandarini na kutafuta eneo mbadala la kuyahifadhi ili kuepuka kuongezeka kwa gharama ya kodi yanapokaa muda mrefu eneo hilo.

Katanga amesema tayari jana Januari 8, walikamilisha upakuaji wa mabasi hayo kutoka kwenye meli.

Amesema yaliyoingia nchini ni kati ya 99 yanayopaswa kuletwa ili kuboresha huduma ya usafiri katika barabara ya Kimara ambayo ni awamu ya kwanza ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-1). Mradi huo ulianza kufanya kazi mwaka 2016.

Hata hivyo, mradi huo unaopaswa kuwa na mabasi 305, ulisalia na 40 pekee yanayofanya kazi baada ya mengine kuharibika.

Hatua hiyo ilielezwa kuchangiwa na kufanya kazi muda mrefu bila ya matengenezo na kubeba abiria kupita uwezo wake.

Ni kutokana na hali hiyo, wananchi kwa nyakati tofauti walipaza sauti kuhusu huduma mbovu ya mabasi hayo inayosababisha wakae muda mrefu vituoni.

Serikali ilitangaza kuongeza mabasi 60 ambayo ni kutoka mradi huo njia ya Mbagala yaliyo chini ya Kampuni ya Mofat.

Uamuzi huo ulitangazwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Oktoba 2, 2025, alipofanya ziara kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri wa mabasi hayo Kivukoni hadi Kimara jijini Dar es Salaam.

Majaliwa alisema Serikali iliamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye barabara hiyo iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu wa uliokuwepo.

“Tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka Kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo (Oktoba 2), malengo yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 9, 2026, Katanga amesema mabasi mengine 50 yanatarajiwa kuletwa Januari 15, hivyo kufanya jumla ya mapya kufikia 100. Moja la mfano lilishaingia nchini na tayari linafanya kazi.

“Kabla ya kutokea changamoto kulikuwa na mabasi 140, baadaye yaliharibika kwa sababu ya kutumika muda mrefu bila ya kufanyiwa matengenezo, kukumbwa na mafuriko pale Jangwani, lakini yapo yaliyochomwa moto kipindi cha vurugu za uchaguzi (Oktoba 29, 2025) na kufanya mabasi 40 tu ndio yafanye kazi,” amesema na kuongeza:

“Hivyo ujio wa mabasi hayo utasaidia kuboresha usafiri katika Barabara ya Kimara ambako wananchi wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu.”

Katanga amesema: “Pia, tayari Serikali ilishatoa Sh1.2 bilioni kwa ajili ya kukarabati mabasi mengine 30, mpaka sasa mabasi 20 yameshakarabatiwa tayari kuanza kazi. Tuna imani wananchi watafurahia huduma zetu.”

Amewashukuru wananchi kwa uvumilivu katika kipindi chote kulipokuwa na changamoto, akiahidi siku za usoni wataona huduma bora zikitolewa na kampuni hiyo.

Vilevile, amewataka wananchi kuyatunza mabasi hayo.

Mkazi wa Kimara, Raphael Chirwa amesema Udart pia wanapaswa kuyatunza mabasi hayo kwa kuwa yamenunuliwa kwa kodi za wananchi.

“Kuna tabia ya baashi ya watumishi hawajali wakiona mradi ni wa Serikali, hivyo kutokuwa makini kuangalia mali husika,” amesema.

Kwa upande wake, Neema Dawson, mkazi wa Mbezi, amesema ahadi ya kutolewa huduma bora iende kwa vitendo kwa kuwa hata waongezewe mabasi 500 kama hawatakuwa tayari kujituma na kujisimamia haitasaidia.