Barker afichua matatizo ya Simba SC

JANA Alhamisi, Simba ilichapwa bao 1-0 na Azam FC matokeo yaliyohitimisha safari yao katika Kombe la Mapinduzi 2026, lakini huku nyuma kocha mkuu wa kikosi hicho, Steven Robert Barker ametoa kauli nzito akifichua matatizo yaliyopo ndani ya timu hiyo.

Siku moja kabla ya mechi hiyo, Barker amesema kucheza dhidi ya Azam FC kwake ni kipimo sahihi cha kujua utayari wa kikosi chake kuelekea mechi za CAF dhidi ya Esperance.

Baada ya mechi, akaibuka kwa kutaja matatizo yaliyopo ambayo amepanga kuyapatia dawa kabla ya Januari 24, 2026 kucheza ugenini dhidi ya Esperance katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa mkiani mwa kundi D bila pointi.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alitaja matatizo yaliyopo ndani ya Simba yanachangiwa na maeneo matatu, ulinzi kushindwa kuzuia kikamilifu mipira ya kutengwa, kiungo kutengeneza mashambulizi ya kutosha na ushambuliaji kushindwa kulazimisha kuvunja safu ya wapinzani.

“Ndiyo, kwa wazi kabisa, ni jambo la kuvunja moyo kila unapopoteza mechi yoyote, na hasa zaidi unapopoteza nusu fainali. Kusema ukweli, kikosi kilirejea wiki iliyopita Jumanne. Tumekuwa pamoja kwa wiki moja tu. Hii ni mechi yetu ya tatu ndani ya wiki moja. 

“Baadhi ya wachezaji wetu muhimu kama (Elie) Mpanzu na (Steven) Mukwala walijiunga na timu siku moja au mbili zilizopita tu. Kwa hiyo imekuwa kipindi kigumu kuwakusanya wote, kuwaunganisha na kuwafanya wacheze kwa namna tunayotaka,” amesema Barker.

Msauzi huyo alieleza kwamba hali ya utimamu katika kikosi chake haipo sawa, hivyo kuna ulazima wa kushughulikia hilo.

“Niwe muwazi hali ya utimamu wa miili siyo kama tunavyotaka kutokana na namna tunavyokusudia kucheza. Hivyo usiku wa leo (juzi) ilikuwa kama vita ya kuteseka kimwili,” amesema.

DU 02

Barler amesema: “Katika mechi zote tatu tulizocheza (dhidi ya Muembe Makumbi, Fufuni na Azam), hatujatengeneza nafasi za kutosha. Hatutengenezi nafasi nyingi, hatuvuki safu ya ulinzi mara nyingi ili kuwaumiza wapinzani. Hili ni eneo muhimu kwangu kulifanyia kazi na kuliboresha kwa sababu kama tunataka kufanikisha malengo yetu kama klabu, tunatakiwa kuwauliza wapinzani maswali mengi zaidi. 

“Nilihisi kwamba katika mchezo huu (dhidi ya Azam), wao (Azam) walikuwa na hatari zaidi kupitia mipira ya kutengwa (set pieces). Kwa wazi wana wachezaji warefu, na tulikuwa tunatoa nafasi nyingi zisizo za lazima katika eneo letu la hatari.

“Hilo lilikuwa jambo la kukatisha tamaa. Pia, baada ya kufungwa bao, ndipo timu ikaanza kuonesha nguvu na mwitikio, jambo ambalo silitaki. Sitaki tusubiri kufungwa ndipo tuanze kucheza kwa nguvu na ari. 

“Tunapaswa kuanza mechi kwa nguvu hiyohiyo na kuicheza dakika 90 kwa mtindo huohuo. Kwa hiyo, kuna hali ya kuvunjika moyo, lakini pia ni muhimu kama funzo. 

NAB 01

“Tunapaswa kurudi kazini. Nahitaji kuiweka timu katika nafasi bora zaidi kiufundi na kimwili. Tuna mechi kubwa inayokuja hivi karibuni (dhidi ya Esperance), kwa hiyo kipindi hiki kinatupa fursa ya kurejea, kuwarudisha wachezaji wa timu ya taifa, na kuwafikisha katika kiwango bora cha kuelewa namna ninavyotaka wacheze. 

“Katika vipigo, kuna mengi ya kujifunza. Na naamini hata leo (jana), nimejifunza mengi. Na mambo mengi yaliyojitokeza hayatotokea tena,” amesema Barker.

Kwa sasa, Barker ana kazi ya kufanya kutatua matatizo hayo zikibaki siku 14 kabla ya kucheza na Esperance nchini Tunisia, kisha kurudiana wiki moja mbele jijini Dar. Mechi hizo zimeshikilia hatma ya Simba kufuzu robo fainali kwani ikipoteza, itakuwa imeumaliza mwendo.