Kiungo Simba amtaja Fei Toto, Ajibu

KIUNGO wa zamani wa Simba, Azam FC na Taifa Stars, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ amesema ikitokea akapewa nafasi kuchagua nyota wa sasa akapangwa kucheza naye mechi katika timu moja, basi fursa hiyo itwaangukia Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Ibrahim Ajibu.

Redondo ni mmoja kati ya wachezaji mahiri ambao waliwika kwenye soka la Tanzania akiwa anatajwa kuwa mmoja kati ya viungo wenye mbwembwe nyingi akiwa uwanjani, lakini ni kati ya wale ambao walifanikiwa kucheza soka kwa muda mrefu.

Mkongwe huyo amesema Fei Toto wa Azam ambaye msimu wa 2023/24 alimaliza na asisti saba, huku 2024/25 akimaliza nazo 13 na huu ana moja, na ni mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye ligi pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

“Kuna wachezaji wengi mafundi katika nafasi hiyo, lakini Ajibu na Fei Toto wana uwezo wa kukupa vitu vingi uwanjani ambavyo vinaweza vikarahisisha mechi ngumu na mkapata matokeo ya ushindi,” amesema Redondo na kuongeza:

“Nikicheza nao katika mechi moja hapo ni kugawana  majukumu, mwingine anaweza akacheza nane mwingine 10 na mwingine akatokea pembani, hizo pasi zitakazotembezwa wapinzani watalala na viatu.”