DK Nchimbi: Maendeleo ya elimu Zanzibar ni tunda la Mapinduzi

Unguja. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema malengo makuu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalilenga kuboresha maisha ya wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii, malengo ambayo kwa kipindi cha miaka 62 yamefanikiwa kutekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Ijuma Januari 9, 2026, wakati akifungua Shule ya Msingi Makunduchi mkoani Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema miradi na hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar ni utekelezaji wa ndoto za waasisi wa Mapinduzi, waliokusudia kuwaletea wananchi huduma bora za kijamii na kuinua maisha yao.

Akizungumzia hali ya elimu kabla ya Mapinduzi, Dk Nchimbi amesema Wazanzibari wengi waliishi katika mazingira duni huku fursa za elimu zikiwa chache, akieleza kuwa kulikuwa na shule 68 pekee zenye jumla ya wanafunzi wapatao 25,000 waliopata nafasi ya masomo kwa misingi ya ubaguzi.

Amebainisha kuwa ndani ya miaka 62 ya Mapinduzi, sekta ya elimu imepata mabadiliko makubwa, ambapo idadi ya shule imeongezeka hadi kufikia 1,200 kutoka shule 68 zilizokuwapo awali, huku wanafunzi wakiongezeka hadi zaidi ya 600,000.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na wafanyakazi na wananchi wa Makunduchi baada ya kufungua Shule ya Sekondari Makunduchi Mkoa wa Kusini, Unguja.

“Kabla ya Mapinduzi Zanzibar hakukuwa na chuo kikuu hata kimoja, lakini kwa sasa kuna vyuo vikuu vitano, hatua hii ni ushahidi wa utekelezaji wa malengo halisi ya Mapinduzi ya kuondoa ukoloni na kuleta maendeleo kwa wananchi,” amesema makamu huyo wa Rais wa Tanzania.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya mitalaa ya elimu kwa kuzingatia ufundishaji wa vitendo na ubunifu, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa.

Pia, Dk Nchimbi amesema miundombinu ya elimu imeimarishwa kwa kutumia teknolojia za kisasa, jambo linalorahisisha ufundishaji na kuongeza uelewa kwa wanafunzi.

Hata hivyo, amesema mabadiliko ya mitalaa  yameanzisha mikondo miwili ya elimu, mkondo wa kawaida na mkondo wa amali, lengo likiwa ni kutoa fursa kwa kila mtoto kunufaika na elimu kulingana na uwezo na mwelekeo wake. Katika hafla hiyo, Dk Nchimbi amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa jitihada zao zilizochangia kupatikana kwa maendeleo hayo.

Akizungumzia Muungano, Makamu wa Rais amesema ndani ya miaka 62, matunda ya Muungano yameonekana wazi kwa kuimarisha uhuru, umoja, maendeleo na amani ya Taifa. Amewataka wananchi kuendelea kulinda na kuenzi amani, akisisitiza bila amani hakutakuwa na mshikamano wala maendeleo endelevu.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Amida Mussa alisema mkoa huo ulikuwa nyuma kimaendeleo katika sekta ya elimu kutokana na upungufu wa miundombinu.

Amesema hali hiyo  imesababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi madarasani.

Amida amesema shule nyingi zililazimika kuendesha mikondo miwili, huku darasa moja likiwa na zaidi ya wanafunzi 75, lakini kwa sasa shule zinaendesha mkondo mmoja pekee na idadi ya wanafunzi imepungua hadi chini ya 45 kwa darasa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdallah Said amesema kabla ya ujenzi wa Shule ya Msingi Makunduchi, kulikuwapo shule kongwe iliyojengwa zaidi ya miaka 103 iliyopita ambayo ilikuwa imechakaa.

Amesema ujenzi wa shule hiyo umeweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.

Amesema mradi wa ujenzi wa shule hiyo umegharimiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo ujenzi ulianza mwaka 2023 na kukamilika Desemba 2025 kwa gharama ya Shilingi bilioni 6. Shule hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,890 na ina jumla ya vyumba 42 vya madarasa vyenye wastani wa wanafunzi 45 kila kimoja, vyoo 52, ofisi ya mwalimu mkuu, ofisi nne za walimu, ukumbi wa mitihani, maabara za kisasa, chumba cha kompyuta na chumba cha ushauri nasaha.

Ameongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo utaondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika eneo la Makunduchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema changamoto ya msongamano wa wanafunzi haikuwa ya Makunduchi pekee bali ilikuwa ni tatizo kwa Zanzibar nzima. Alisema mchango wa Muungano hauwezi kubezwa, akibainisha kuwa fursa mbalimbali zimeendelea kutolewa kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano, ikiwemo fursa kwa vijana wa Zanzibar kupata mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka Tanzania Bara.