Matumizi ya pombe yapaa mihadarati ikipungua mtaani

Dar es Salaam. Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya kiasi cha dawa hizo kutotonekana tena kwa uwazi mitaani, hali ambayo imeleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiusalama.

Hata hivyo, mafanikio hayo sasa yanaambatana na changamoto mpya ya kuongezeka kwa ulevi wa pombe kupita kiasi, hususan miongoni mwa vijana waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo leo Januari 9, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya mamlaka hiyo na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.

Kikao hicho kililenga kujadili hali ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya na nafasi ya vyombo vya habari katika vita hivyo.

Lyimo amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo dawa kama heroini na cocaine zilikuwa zikiuzwa waziwazi mitaani.

Amesema hali hiyo ilisababisha jamii kuzoea uwepo wa dawa hizo kiasi cha hata wafanyabiashara wake kutajwa na kuimbwa kwenye nyimbo za bendi za muziki.

“Kwa sasa mtaani hakuna dawa za kulevya kama heroini na cocaine pamoja na dawa nyingine hatarishi. Mafanikio haya yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi,” amesema Lyimo.

Ameongeza kuwa maneno na misamiati iliyokuwa ikitumika na watumiaji na wauzaji wa dawa hizo, kama vile ‘Zungu la Unga’, haipigiwi tena masikioni, ishara kwamba biashara hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa Lyimo, hali ya sasa ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo mitaa mingi ilitambulika kama maeneo ya wazi ya biashara ya dawa za kulevya.

Akizungumzia usalama wa mipaka, Kamishina Jenerali huyo amesema Tanzania siyo tena mlango wa kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi nyingine, baada ya mianya yote iliyokuwa ikitumiwa na wahalifu kufungwa.

Amesema mafanikio hayo yamechangia hata kupungua kwa ukaguzi mkali wa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege, tofauti na ilivyokuwa awali.

“Zamani Watanzania walikuwa wanakaguliwa sana viwanjani kwa hofu ya kusafirisha dawa za kulevya, lakini sasa hali hiyo imepungua kwa sababu nchi imeonesha mafanikio makubwa katika kudhibiti tatizo hilo,” amesema.

Hata hivyo, Lyimo amesema ushindi huo umeacha pengo ambalo sasa linajazwa na tatizo la ulevi wa pombe kupindukia.

Kwa mujibu wake, vijana wengi waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya wamehamia katika matumizi makubwa ya pombe, hali inayohitaji nguvu mpya katika mapambano ya afya ya jamii.

Amesema DCEA kwa sasa ina jumla ya nyumba za upataji nafuu (sober house) 78 nchini, na kwa sehemu kubwa soba hizo zimejaa waraibu wa pombe.

Hali hiyo, amesema, ni ishara kwamba ulevi umeanza kuchukua nafasi ya dawa za kulevya kama tishio jipya kwa ustawi wa jamii.

“Baada ya kukosekana dawa za kulevya, vijana wengi wameingia kwenye ulevi. Hii inatulazimu sasa kuweka mkazo mkubwa katika mapambano dhidi ya ulevi wa kupindukia, sambamba na kuhamasisha waraibu kujiunga na soba ili kupata tiba,” amesema.

Kamishina Jenerali Lyimo amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya na ulevi hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa jamii nzima, wakiwemo wazazi, viongozi wa dini, serikali za mitaa na vyombo vya habari.

Ameeleza kuwa elimu kwa umma na mabadiliko ya mtazamo ni silaha muhimu katika kudhibiti matatizo hayo.

Kuhusu kikao kazi hicho, Lyimo amesema DCEA inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kupambana na dawa za kulevya.

Amesema waandishi wa habari ni washirika muhimu katika kuibua taarifa, kuelimisha jamii na kushawishi mabadiliko chanya ya tabia.

“Waandishi wa habari ni sehemu ya suluhisho katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Ndiyo maana tumeona umuhimu wa kukutana nao, kujengana uwezo na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu na mikakati itakayosaidia kuboresha zaidi mapambano haya,” amesema Lyimo.

Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa gazeti la Nipashe Salome Kitomari amesema vyombo vya habari zina nafasi kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya akiwataka wanahabari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii dhidi ya dawa hizo haramu.

“Sisi kama wana habari tunaweza kuwa na mchango mkubwa katika vita hii, tunachohitaji ni ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mamlaka katika kuhakikisha tunapata taarifa, tunawafikia waathirika na tunafikisha ujumbe kwa jamii,” amesema Salome.