Wafanyakazi wa shamba la maua wagoma, kisa masilahi

Moshi. Mamia ya wafanyakazi wa shamba la maua la Vaso Agro-ventures Ltd, lililopo Kibosho, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wamegoma kufanya kazi, wakishinikiza uongozi kupandisha mshahara kuendana na kima cha chini kilichopangwa na Serikali kwa sekta binafsi.

Katika mgomo huo uliofanyika leo, wafanyakazi hao waliondoka maeneo yao ya kazi na kukusanyika eneo moja wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali, ikiwemo kushinikiza nyongeza ya mishahara na kutaka kujua hatma yao.

Kufuatia mgomo huo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Azizi Kalokola, alifika katika eneo hilo na kuwatuliza wafanyakazi hao ambao walikuwa wamegoma tangu asubuhi.

Licha ya waandishi wa habari kufika katika Ofisi za shamba hilo, viongozi waliokuwepo hawakuwa tayari kuzungumzia malalamiko hayo kwa madai kuwa msemaji hayupo, na hata namba ya simu waliyotoa kuwasiliana na mhusika haikupatikana hewani.

Wakizungumza baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, walisema mishahara wanayolipwa ni midogo na mazingira ya kazi ni magumu, hali ambayo imedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Prosper Massawe alisema mshahara haukidhi mahitaji kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

“Tunacholalamikia ni mishahara midogo na manyanyaso kazini. Tunataka mshahara uongezeke ili kuendana na hali halisi ya maisha kwa sasa,” alisema Massawe.

Aliongeza kuwa kwa sasa wanalipwa mshahara wa Sh157,000, huku kukiwa na ahadi ya kuongezewa Sh18,000 ili kufikia Sh175,000, lakini utekelezaji haujaanza ipasavyo.

Pia, alibainisha kuwa wanafanya kazi katika mazingira hatarishi yenye sumu huku wakikatwa makato yasiyoeleweka kama gharama za benki, chai, na chakula.

Mfanyakazi mwingine, Mary Kulaya, alieleza kuwepo kwa mfumo wa malipo unaozua mkanganyiko ambapo baadhi hulipwa tarehe 12 na wengine tarehe 30 ya mwezi.

“Tulipewa barua ya kuongeza mshahara, lakini sisi tunaolipwa tarehe 12 tunaambiwa bado tunalipwa Sh157,000 badala ya Sh175,000 kama ilivyoelekezwa,” alisema Kulaya.

Kulaya amesema walipohoji

sababu ya kuchelewa kuanza kulipwa mshahara mpya, waliambiwa kuwa wiki mbili za Januari zinahesabiwa kuwa za Desemba, hivyo mshahara wa Sh175,000 utaanza

kulipwa Februari, jambo ambalo wafanyakazi wanalipinga.

Kwa upande wake, Ushindi Paulo alilalamikia makato ya hifadhi ya jamii (NSSF/PSSSF). Alidai kuwa licha ya kukatwa fedha kila mwezi, michango hiyo haionekani kuwasilishwa kwenye mifuko husika.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa shamba hilo, Hussein Abdallah amekiri kuwa mazungumzo na menejimenti hayajazaa matunda bado.

“Tulifanya maridhiano kuhusu ajenda za wafanyakazi lakini tulishindwa kufikia mwafaka. Tumepeleka suala hili ngazi ya juu ya kanda na wamesema wanashughulikia,” alisema Abdallah.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Azizi Kalokola, aliwataka wafanyakazi hao kuwa watulivu wakati serikali ikitafuta suluhu

“Nimeshamfikishia Kamanda wa Polisi wa Mkoa ambaye amewasiliana na Mkuu wa Mkoa ili suala hili lipate ufumbuzi. Mkuu wa Mkoa atawasikiliza wote ili kupata suluhu ya haraka,” alihitimisha OCD.