Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amehimiza kufanya uwekezaji mkubwa katika hoteli za kitalii kwa lengo la kuchochea shughuli za utalii na kupanua wigo wa mapato na ajira.
Rais Samia ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 9, 2026 wakati akifungua hoteli ya Jaz Elite Aurora, iliyoko Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea sherehe za miaka 62 ya Mapinduzi.
Akihutubia mamia ya waliohudhuria katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema sekta ya utalii imekuwa nguzo muhimu katika kuchochea uchumi na kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini.
“Uwekezaji katika sekta hii ni muhimu sana, maana unachangia kuleta mabadiliko na kukuza uchumi wa taifa na mtu mmojammoja,” amesema Rais Samia.
Amesema serikali zote mbili zinaendele kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuwavutia wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika kipindi cha miaka mitano, amesema sekta ya utalii imeajiri watanzania zaidi ya 2.5 milioni.
Kwa mujibu wa Rais Samia, watalii wameendelea kuongezeka nchini na wamefikia milioni tano mwaka jana, ikilinganishwa na watalii milioni moja walioingia mwaka 2020 huku mapato yakiongezeka na kufikia Dola 4.2 bilioni za Marekani.
Pia, amesema waongoza watalii nao wameongezeka kutoka zaidi ya 5,000 na kufikia zaidi ya 7,000.
Akizungumza kuhusu Zanzibar pekee, amesema watalii kwa mwaka 2024 waliotembelea walikuwa zaidi 743,000 na sasa wamefikia 816,000.
Amesema kwa upande wa hoteli, Zanzibar zilikuwapo takribani 400 na zimekuwa zikiongezeka na hizi zinazoendelea kujengwa, zitakuwa nyingi zaidi kwa ajili ya kuendeleza utalii.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, baada ya nchi kufunguka na jitihada walizofanya, utalii umeongezeka kwa kasi kubwa.
Rais Samia amesema licha ya uwekezaji huo kukua, lazima uende sambamba na uzingatiaji wa uhifadhi wa bahari na fukwe ili kuendelea kupata wawekezaji wengi zaidi.
Katika uendeshaji wa hoteli hizo, amesema Serikali zote mbili zinapaswa kuwahimize wawekezaji kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuwapa fursa wazalishaji wa ndani kuuza bidhaa hizo ili waongeze mapato yao.
“Tukifanya hivyo, tutapunguza fedha kuagiza matunda na bidhaa zingine kutoka nje ya nchi kwa ajili ya hoteli zetu,” amesema Rais Samia.
Amezitaka wizara husika kulisimamia hilo ili wananchi wanufaike na uwepo wa hoteli zinazojengwa nchini.
Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu nchini.
“Wanaotaka kuvunja amani ya nchi yetu, niwasihi acheni mara moja, maendeleo yetu ni pale unapoamka salama, tutunze amani yetu tofauti za mawazo zipo lakini tulinde amani yetu,” amesema Rais Samia
Awali, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff alisema miongoni mwa mafanikio yaliyopitikana ni kuongezeka kwa miradi ya kimkakati zikiwamo hoteli za hadhi za kimataifa.
Amesema ongezeko hilo zitasaidia kuleta ushindani na ubora wa huduma kwa hadhi ya Zanzibar katika soko la utalii kimataifa.
“Uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali kuongezeka kwa mchango wa sekta binafsi na kupanuka kwa ajira kwa wananchi wa Zanzibar, vijana na wanawake,” amesema Shariff.
Amewapongeza wawekezaji hao kwa kuendelea kuwekeza katika maeneo tofauti visiwani humo.
Kwa mujibu wa Shariff, sheria na sera vilivyopo sasa vinaendelea kushawishi wawekezaji kuendelea kuwekeza kwa wingi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema hoteli hiyo inagharimu Dola 35 milioni za Marekani (Sh86.4 bilioni).
Saad amesema tangu mwaka 2020 mpaka sasa Zipa imesajili miradi 528 ikiwa na thamani ya Dola 6.9 bilioni za Marekani (Sh17.1 bilioni) yenye uwezo wa kutoa ajira 25,000.
Amesema Mkoa wa Kusini Pekee, umesajili miradi 240.
“Zanzibar tunaendelea kupokea wawekezaji mbalimbali tukilenga kukuza uchumi wa taifa na wa mtu mmojammoja,” amesema.