Mama mdogo adaiwa kumjeruhi mwanaye kisa koti

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro, linamshikilia mwanamke mmoja, mkazi wa kiijiji cha Ongoma Kusini, kata ya Uru Kaskazini, Wilaya ya Moshi kwa tuhuma za  kumjeruhi mtoto wa dada yake akidai kumchukulia koti lake na kulivaa.

Inadaiwa kuwa Januari 4, 2026  mtoto huyo  wa kiume ambaye ni  wa darasa la tano katika shule moja iliyopo kijijini hapo, alichukua koti hilo na kulivaa ili kujisitiri baridi hali ambayo iliyomchukiza mama yake mdogo na kuanza kumshambulia kwa kutumia kitu butu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa mwanamke huyo ambaye hajamtaja kwa jina Januari 6, 2025 na kwamba taratibu za kiuchunguzi zinaendelea na zikikamilika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Ni kweli tunamshikilia mwanamke mmoja kwa kufanya tukio la shambulio la mwili kwa mtoto huyo, taratibu zetu za kipolisi zikikamilika tutamfikisha mahakamani,” amesema Kamanda Maigwa.

Mtoto mwenyewe asimulia ilivyokuwa

Akisimulia mtoto huyo, amesema siku ya tukio alikutana na vijana wawili ambao walidai kutumwa na mama yake mdogo wamkamate, ndipo vijana hao walipomkamata na kumpeleka nyumbani kwa mama yake huyo mdogo.

“Siku  ya Jumapili nilichukua tuu koti la mama mdogo, nilikuwa naskia baridi nikalivaa, baada ya kulivaa,  asubuhi nikarudisha  ili niende kwa bibi, wakati narudisha nikakutana na wakaka, wakanambia tumeambiwa tukutafute nikasema haya, wakanichukua wakanifikisha nyumbani, nilipofika mama alinipiga na nondo za kichwani, nilipomwonyesha koti lilipo ndipo akanichoma na plastiki lenye moto kwenye mikono,” amesema mtoto huyo.

Akizungumzia tukio hilo, babu wa mtoto huyo, Frate Mushi amesema tukio la kufanyiwa ukatili mjukuu wake linatokana na kuchukua koti la mama yake mdogo na kulivaa bila ridhaa yake.

Amesema Jumapili usiku wakati akirejea nyumbani akitokea Njoro, Moshi Mjini, alimkuta  mtoto huyo akiwa katika hali mbaya kiafya, akilalamika maumivu makali kichwani, mbavuni na mkononi, huku mwili wake ukiwa umeloweshwa maji.

“Mjukuu wangu alikuwa amekaa kwenye kochi, hawezi hata kujigusa. Aliniambia kichwani amepigwa na mkononi amechomwa kwa nailoni, nilishangaa sana kwa sababu hakuna aliyenieleza chochote kabla ya kumuona mjukuu wangu akiwa katika maumivu makali,” amesema mzee Mushi.

Naye, Sarapia Mushi,  ambaye ni bibi wa mtoto  huyo amesema alibaini mjukuu wake huyo kuumizwa wakati alipomfungilia mlango akiwa anajiburuza kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo.

“Siku ya tukio nilienda kumtembelea shangazi wa mume wangu huko Njoro, wakati narudi nyumbani  nikauliza mbona hawawashi taa ndani, tukagonga mlango baadaye tukaona mtoto anatambaa kwa kujiburuza na kufungua mlango, tulimuuliza ni nini akasema mama mdogo ndio kampiga na kisha akamaleta nyumbani kwangu na kumtelekeza,”ameeleza bibi huyo.

Amesema “Nilijitahidi kumuogesha lakini alikuwa analalamika maumivu makali sehemu za nyonga, kiunoni na kichwani, kesho yake ilibidi nikatoe taarifa polisi na ndipo nilipopata msaada mhusika akakamatwa.”

Aidha, amesema tukio hilo halileti taswira nzuri kwa jamii kwani mtoto huyo alikuchukua koti hilo kujisitiri baridi na si vinginevyo.