SHIRIKA LA MASOKO YA KARIAKOO, SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI JESHI LA POLISI WAKUTANA KUJADILI MIKAKATI YA ULINZI SOKO LA KARIAKOO.

Shirika la Masoko ya Kariakoo limefanya kikao maalum na uongozi wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi ambalo linatoa huduma za ulinzi katika soko la Kariakoo, kikao ambacho kimelenga kujadili namna bora ya kuimarisha ulinzi sokoni hapo.

Akiongea katika kikao hicho Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA. Ashraph Abdulkarim amesema kufanyika kwa kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya ufunguzi wa soko hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 99.

“Ni wajibu wetu kuona ni kwa namna gani kila mdau amejipanga kutoa huduma bora kwa wananchi na kufanya maboresho stahiki kabla ya ufunguzi wa soko, kwani litakapofunguliwa litajumuisha watu wengi ambao ulinzi wao pamoja na mali zao unatakiwa kuimarishwa na kuwa bora zaidi” ameongeza CPA. Abdulkarim.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Shirika la Masoko ya Kariakoo ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wanapata huduma bora kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Aidha, amelishukuru Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa kuwapatia mafunzo ya huduma bora kwa mteja kwa askari wa shirika hilo la Polisi na kuongeza kuwa mafunzo hayo yameongeza chachu ya utendaji kazi na uwajibikaji wa askari wake.