Na.Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) imesema imeendelea kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi, ili kuhakikisha wananchi wananufaika na shughuli za uchimbaji na utafutaji.
Akizungumza jijini Dar es salam jana katika mahojiano maalum,Katibu Mtendaji wa TEITI, Bi. Mariam Mgaya, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 57 zinazotekeleza viwango vya kimataifa vya uwazi na uwajibikaji vinavyosimamiwa na EITI.
Amesema Tanzania ilijiunga na EITI mwaka 2009, hatua iliyolenga kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa maslahi ya maendeleo endelevu.
“Asasi hii inahamasisha wananchi kuelewa hatua zote za mnyororo wa thamani wa rasilimali hizi, ikiwemo ukusanyaji na ufuatiliaji wa mapato,” amesema Bi.Mgaya
Bi. Mgaya amebainisha kuwa utekelezaji wa majukumu ya TEITI unasimamiwa na Sheria ya TEITA ya mwaka 2015 ambayo imeainisha jukumu la kuboresha uwazi na uwajibikaji, hasa katika uvunaji wa rasilimali hizo.
Aidha, ameeleza kuwa mpaka sasa TEITI imechapisha ripoti 15 zinazolinganishwa kati ya malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi na mapato ya Serikali, kuanzia Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2023.
“Uwekaji wazi wa ripoti hizi ni sehemu ya utekelezaji wa viwango vya kimataifa ambapo nchi wanachama hutakiwa kufichua takwimu zote za mnyororo wa thamani,” ameongeza.
Hata hivyo Bi. Mgaya ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuiwezesha TEITI kifedha na kimiongozo ili kuhakikisha rasilimali za madini, mafuta na gesi zinaendelea kunufaisha wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwazi na Uwajibikaji, Bw. Erick Ketagory, amesema TEITI inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu taarifa zinazochapishwa kwenye ripoti hizo na namna zinavyoweza kutumika kuibua mijadala kuhusu manufaa ya rasilimali za nchi.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka wazi huduma 20 muhimu zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 katika migodi, akitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizo.
Ketagory ameongeza kuwa TEITI ina wajibu wa kuhakikisha kampuni za uchimbaji na utafutaji zinatoa taarifa za shughuli zao kwa mujibu wa sheria, sambamba na kujenga uwezo wa wananchi kutumia takwimu hizo kuhoji na kufuatilia uwajibikaji.
“Ripoti za TEITI ni nyaraka muhimu sana kwa sababu zinaweka wazi malipo ya kodi na tozo mbalimbali zinazolipwa serikalini,” amesisitiza.