Mbeya. Diwani wa kata ya Ruanda jijini Mbeya, Isack Mwakubombaki amesema uongozi wake utakuwa wa kuishirikisha jamii huku, akieleza kuwa atakuwa tayari kutumia rasilimali zake kutatua changamoto za wananchi hususani barabara.
Kauli hiyo inakuja kufuatia kilio cha wananchi kulalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara haswa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha na kuleta athari kwa watu.
Kufuatia uwapo wa mvua jijini Mbeya, Jeshi la Zimamoto na uokoaji katika taarifa yake iliyoitoa Januari 3, 2026 ilieleza watu wanne wanadaiwa kufariki dunia baada ya kusombwa na maji, huku likitoa tahadhari kwa wananchi kuchukua tahadhari.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 9, diwani huyo amesema hataisubiri serikali kutatua changamoto, bali uongozi wake utakuwa wa kuishirikisha jamii kuhakikisha kero zilizo ndani ya uwezo wake anazimaliza.
Amesema atakuwa tayari kutumia aina yoyote ya rasilimali aliyonayo yakiwamo magreda ya kuchonga barabara anayoyamiliki, kuhakikisha changamoto za barabara katika kata yake zinatatuliwa.
“Ninaongoza kata iliyopo kwenye jiji ambayo wageni na wananchi wengi wanafikia, lazima tujitolee na ndio wajibu na sababu za kuomba ridhaa za kuwatumikia wananchi, sitasubiri kila kitu serikali ikifanye,” amesema.
“Nina nyenzo za kusaidia baadhi ya shughuli kama greda zangu na ninaweza kutumia chochote kuhakikisha naboresha hizi barabara za pembezoni kwa kushirikiana na Tarura” amesema Mwakubombaki.
Diwani huyo ameongeza kuwa matarajio yake kwa kipindi cha miaka mitano ni kuwafungulia fursa vijana za kichumi ili kuondoa makaundi mtaani akieleza kuwa kiu yake ni kuona kila mwananchi anakuwa na kazi inayomuingizia kipato.
“Wapo baadhi ya wadau natarajia kukutana nao kujadiliana nao namna ya kutengeneza mifumo ya vijana wetu wasikae mtaani bila kazi za kufanya, nataka kila mwananchi wa Kata ya Ruanda awe na shughuli ya kumuingizia kipato” amesema Diwani huyo.
Mmoja wa wananchi katika Kata hiyo, Jeremiah Jonas amesema kero kubwa kwa sasa ni vijana kukosa kazi, changamoto ya barabara na maji safi, akiomba serikali kuangalia uwezekano wa kumaliza kero hizo.
“Vijana wapewe mikopo wafanye shughuli binafsi, serikali isaidie maeneo yenye changamoto mfano huduma ya maji na barabara viwe rafiki pamoja uhakika wa umeme ili kazi zisikwame” amesema Jonas.
Naye Huruma Jason mkazi wa Soweto amesema ipo kero kwenye mifereji ambayo baadhi yake huleta changamoto ya maji kwenye makazi ya watu pale mvua inaponyesha akiomba kufanyiwa kazi.
“Tupo kwenye msimu wa mvua, kuna baadhi ya mifereji inatapisha maji hadi kwenye makazi ya watu, tunaomba itazamwe lakini suala la maji nayo ni changamoto kubwa, ifanyiwe kazi” amesema Huruma.