WAHITIMU wa mafunzo ya udereva wa barabarani yaliyofadhiliwa na Mbunge wa Jimbo la Ukonga wameiomba Serikali kuwapatia mikopo ili waweze kununua pikipiki na bajaji kwa ajili ya kujiajiri, pamoja na kusaidiwa upatikanaji wa leseni kwa gharama nafuu.
Ombi hilo limetolewa wakati wa sherehe ya kugawiwa vyeti iliyofanyika Januari 8, 2026, katika Uwanja wa Pugu, Kata ya Pugu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Edward Mpogolo.
Akizungumza katika hafla hiyo, DC Mpogolo amesema amepokea ombi la wahitimu hao na kuahidi kuwa Serikali iko tayari kuwashika mkono, hususan kwa kusimamia upatikanaji wa mikopo ya halmashauri kwa urahisi ili kuwawezesha kufanikisha ndoto zao za kujiajiri.
“Nampongeza Mbunge wa Jimbo la Ukonga, shemeji yangu Bakari Shingo, kwa kazi kubwa ya huruma aliyofanya kwa vijana wa jimbo hili. Amewasaidia kupata mafunzo kwa gharama zake mwenyewe bila ubaguzi wa wenye nacho na wasio nacho,” amesema DC Mpogolo.
Ameongeza kuwa mikopo ya halmashauri inalenga kuwasaidia wananchi wanyonge, hivyo amewataka watendaji wa Serikali ngazi ya kata kuhakikisha wanawasimamia wahitimu hao pamoja na wananchi wa Ukonga kwa ujumla kupata mikopo hiyo bila urasimu wala vikwazo.
Aidha, kama sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo, DC Mpogolo amewataka wahitimu kuwasilisha majina yao ili ayawasilishe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kusaidiwa kupata punguzo la gharama za ukataji wa leseni.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Bakari Shingo, amesema kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.Ameeleza kuwa wakati akitangaza awali fursa ya mafunzo ya udereva wa pikipiki na bajaji, vijana 350 walijitokeza, lakini kutokana na mwitikio mkubwa idadi ya waliojisajili sasa imefikia 900.
“Naamini Jimbo la Ukonga lina wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Nitawatembelea wote ili tushirikiane, lengo ni kuona namna ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu,” amesema Shingo.