Yanga yaichapa Singida BS, yaifuata Azam fainali Mapinduzi

YANGA imefuzu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya kuifunga Singida Black Stars bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa leo Januari 9, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Maxi Nzengeli ndiye aliyefunga bao hilo dakika ya 54 baada ya kuitumia vizuri pasi ndefu ya mpenyezo iliyopigwa na Pacome Zouzoua kutokea katikati ya uwanja.

Mechi hiyo licha ya kuonekana kuwa na ushindani mkubwa, lakini Yanga ilikuwa imara na kulinda vizuri nyavu zake zisiguswe kwa mara nyingine tena.

Hii ikiwa ni mechi ya tatu kwa Yanga katika michuano hii, kikosi hicho kimefanikiwa kumaliza bila ya kuruhusu bao ikiwa ni timu pekee hadi sasa imefanya hivyo.

Imeshuhudiwa leo kwa mara ya kwanza kadi nyekundu mbili zikionyeshwa katika mechi moja kwa mara ya kwanza wakiadhibiwa Mohamed Damaro wa Yanga na Morice Chukwu wa Singida Black Stars. Hadi sasa zimeonyeshwa kadi nyekundu tatu, baada ya jana beki wa Simba, David Kameta ‘Duchu’ kuwa wa kwanza kuonyeshwa walipofungwa 1-0 na Azam.

Kwa kufuzu fainali, Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Azam, Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, ikisaka taji la tatu baada ya 2007 na 2021.

Azam ambayo imebeba ubingwa huo mara tano ambazo ni 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, ilitangulia fainali baada ya kuichapa Simba bao 1-0, jana Alhamisi Januari 8, 2026.