YANGA bado haijakubali matokeo inamtaka kiungo Allan Okello na sasa bosi mmoja wa juu alikuwa nchini Uganda akipambana na saini ya nyota huyo.
Okello ni mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye kikosi cha Vipers pamoja na timu ya Taifa ya Uganda, akiwa amefanya vizuri kwenye michuano ya CHAN na Kombe la Mataifa Afrika ambako nchi yake iliondolewa hatua ya makundi.
Kuna ofa mbili ambazo Yanga ilituma kwa Vipers ambapo ilianza na kiasi cha Dola 50,000 (takriban Sh 124 milioni) ikakataliwa kisha baadaye ikaongeza mara mbili kufikia Dola 100,000 (takriban Sh248 milioni), lakini nazo zikapigwa chini.
Kugomewa ofa hizo mbili kumemfanya rais wa Yanga, Hersi Said kupanda ndege mpaka Uganda ili akakutane na rais wa Vipers, Lawrence Mulindwa kujadiliana juu ya dili hilo.
Yanga imeishika pabaya Vipers kutokana na klabu hiyo kubakiza miezi sita pekee kwenye mkataba wake na Okello, ambapo endapo Mulindwa atasimamia msimamo ina maana kiungo huyo kuna uwezekano mkubwa akaondoka bure mwisho wa msimu.
Hatua ngumu zaidi kwa Vipers ni kwamba Okello mwenyewe Mwanaspoti linafahamu kwamba mara baada ya kurejea Uganda akitokea Morocco kwenye fainali za Mataifa Afrika, aliwapa msimamo mabosi kwamba anaiheshimu klabu hiyo, lakini anataka kutafuta changamoto mpya.
Hatua hiyo inailazimisha Vipers kujiweka mguu sawa ambapo hata kama dili hilo litakwama sasa, basi uhakika Okello hatavaa jezi nyekundu za timu hiyo msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Okello ameshakubaliana na Yanga kila kitu kwenye mazungumzo ya siri ambapo atasaini dili la miaka miwili na nusu na mshahara mara tatu ya ule anaolipwa Vipers.
Staa mmoja wa Uganda ambaye ni rafiki wa Okello amesema kiungo huyo ameshamaliza makubaliano na Yanga ambapo pia amevutiwa na namna mabingwa hao wa soka wanavyoendelea kubadilika kwa ubora uwanjani.
“Okello amevutiwa sana na Yanga. Unajua ukikutana na viongozi wa Yanga wana akili sana ya ushawishi. Akili yake kwa sasa (Okello) ni Yanga tu. Tulipokuwa naye Uganda kila akitulia anafuatilia taarifa kwenye kurasa zao za kijamii. Ameshashawishika kabisa,” amesema rafiki huyo ambaye pia ni kiungo mkongwe.
“Atakuja tu (Tanzania). Vipers wanatakiwa kupiga hesabu maana hata kama itashindikana sasa miezi michache ijayo ataondoka, ni bora wachukue pesa za Yanga wafanye mambo mengine.”
Yanga inamtaka Okello sasa ikiwa ni mahitaji ya kocha Pablo Goncalves ambaye anatafuta kiungo mahiri namba 10 kwenye kikosi, akitaka kuachana na Mamadou Doumbia ambaye ameshindwa kuonyesha makali kwenye timu hiyo.
Katika msimu huu Okello ndani ya mechi 11 za Vipers inayoongoza Ligi Kuu Uganda amefunga mabao matatu akiwa nyuma ya mshambuliaji Arafat Usama mwenye mabao manne anayeongoza kwa ufungaji ndani ya timu, lakini kiungo huyo akiwa pia na asisti tatu.
