Mradi wa Bridge kunufaisha vijana 1,050

Geita. Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, watanufaika na programu ya mafunzo ya ujasiriamali itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.

Mafunzo hayo yatakayodumu kwa miezi mitatu, yanatolewa kupitia mradi wa Bridge, unaolenga kuwafikia vijana na watu kutoka makundi maalumu 1,050 katika kata 10 za Wilaya ya Geita ifikapo mwaka 2030.

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu tano, katika awamu ya kwanza, vijana 70 wameshaanza kupata mafunzo kwa vitendo.

Kaimu Mkurugenzi Halimashauri ya Wilaya ya Geita, Jonas Kilave akizungumza wakati wa ufunguzi wa program ya mafunzo ya vitendo Kwa vijana.

Mradi wa Bridge unasimamiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) chini ya Tume ya Taifa ya Unesco nchini (TNCU), ukilenga kutoa elimu hiyo.

Kupitia mradi huo, vijana wanatarajiwa kuongezewa ujuzi wa kutambua fursa zilizopo katika mazingira yao na kuzitumia kwa ajili ya kujipatia kipato.

Akizungumza Januari 9, 2026, wakati wa ufunguzi wa mradi huo wilayani Geita, Katibu Mtendaji TNCU, Profesa Hamisi Malebo amesema mradi huo umebeba matumaini makubwa kwa vijana katika kufikia ajenda ya dunia ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

“Mradi huu utakuwa daraja litakalowawezesha washiriki kupiga hatua kutoka ngazi moja hadi nyingine iliyo bora zaidi, kama inavyolengwa na ajenda ya maendeleo endelevu,” amesema Profesa Malebo.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Unesco (TNCU), Profesa Hamis Malebo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa vijana Wilayani Geita.

Profesa Malebo ameongeza kuwa mradi utagusa sekta mbalimbali kama kilimo, usafirishaji, uvuvi na ufugaji, ambazo ni miongoni mwa zinazokua kwa kasi nchini.

Katika kukabiliana na umaskini, profesa huyo amesema Serikali za mitaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, zinaendelea kufanya utambuzi wa makundi yaliyo pembezoni na yaliyo katika mazingira hatarishi, ili kuhakikisha yanapata fursa ya elimu na mafunzo yanayokidhi mahitaji yao kiuchumi.

Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni miongoni mwa halmashauri zitakazonufaika na mradi huo nchini, unaolenga kuwainua kielimu vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 30.

Kati ya wanufaika hao, asilimia 55 watakuwa vijana wa kike na  45 wa kiume.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Jonas Kilave amewataka vijana wanaoshiriki mafunzo hayo kuzingatia nidhamu ya kujifunza na kutumia kikamilifu ujuzi watakaoupata ili uwe chachu ya kuinuka kwao kiuchumi.

“Tunapofungua milango ya programu hii, hatuangalii tu kuanza kwa mafunzo, bali tunaangalia mafanikio makubwa tunayoyatarajia siku za usoni. Tunatarajia miongoni mwa vijana hawa kupatikana wajasiriamali wakubwa na watu wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi,” amesema Kilave.

Katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, vijana walioteuliwa wanapatiwa elimu ya uendeshaji na matengenezo ya pikipiki pamoja na mbinu za kuandaa chakula cha mifugo.

Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo, wameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Unesco kwa kuwasogezea mafunzo ya vitendo, wakisema elimu hiyo itawaongezea ujuzi wa kujiajiri na kuongeza kipato.

“Vijana wengi tupo mtaani bila ajira, hivyo kupitia mradi huu tutaweza kuongeza ujuzi wa kujiajiri na kuboresha maisha yetu,” alisema Happynes Pastory.

Naye Michael Falima amesema mafunzo hayo yatawawezesha vijana kupata maarifa ya vitendo katika fani mbalimbali zenye tija kwao na kwa jamii kwa ujumla.