Marekani. Rais Donald Trump wa Marekani amerejea tena kauli yake ya kutaka nchi yake ichukue udhibiti wa eneo la Greenland, akisema hatua hiyo ni muhimu kwa maslahi ya usalama wa taifa.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa mkutano mrefu uliofanyikia Ikulu ya White House na wakuu wa kampuni za mafuta kuhusu uwekezaji nchini Venezuela hapo jana Januari 9, 2026 kwa mujibu wa BBC.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Trump amesema ana matumaini ya kufikia makubaliano na Serikali ya Denmark kuhusu Greenland, eneo lenye mamlaka ya kujitawala, akisisitiza kuwa umiliki kamili ni muhimu kuliko makubaliano ya muda mrefu ya kijeshi.
“Nchi lazima iwe na umiliki ndipo iweze kujilinda. Huwezi kulinda mikataba ya upangaji,” amesema Trump, akiongeza kuwa endapo Marekani haitachukua hatua, basi China au Russia zinaweza kufanya hivyo.
“Sitaki China au Russia wawe majirani zangu Greenland. Hilo halitatokea,” amesisitiza.
Kauli hizo zimekuja sambamba na mjadala mpana kuhusu mustakabali wa sekta ya mafuta ya Venezuela, chini ya uongozi mpya baada ya kukamatwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo kwa tuhuma za kula njama ya biashara ya dawa za kulevya, tukio lililotokea chini ya wiki moja iliyopita.
Marekani yadhibiti uwekezaji wa mafuta Venezuela
Trump amesema Marekani itatoa dhamana za kiusalama kwa kampuni za Marekani zitakazowekeza Venezuela, akitaja hofu ya mashambulizi dhidi ya kampuni hizo.
Amefichua kuwa meli nyingi za kivita za Marekani (“armada”) zilizopo karibu na pwani ya Venezuela zitatumika kulinda maslahi ya Marekani.
Kwa mujibu wa rais huyo, ni Marekani itakayoamua ni kampuni zipi zitaruhusiwa kufanya kazi nchini Venezuela, akiongeza kuwa chini ya uongozi mpya, nchi hiyo inaelekea kuwa mshirika wa karibu wa Marekani.
Kuhusu mapato ya mauzo ya mafuta, Trump amesema Venezuela itahudumiwa kwanza ili iweze kujiendesha, kampuni za mafuta zilipwe gharama zao, na fedha zitakazosalia zitaelekezwa Marekani.
“Tutahakikisha Venezuela inapata kile inachohitaji kuishi. Baada ya hapo, kutakuwa na fedha nyingi zilizobaki na hizo zitakwenda Marekani, na kampuni za mafuta zitafurahi,”
Alipoulizwa kama kipaumbele chake Venezuela ni utulivu au demokrasia, Trump amesema kwa mtazamo wake mambo hayo ni karibu sawa.
“Tunataka utulivu, lakini pia tunataka demokrasia. Mwisho wa siku, itakuwa demokrasia,” amejibu.
Trump pia ameonyesha kuwa yuko tayari kukutana na viongozi mbalimbali wa Venezuela, akiwemo kiongozi wa upinzani María Corina Machado, anayetarajiwa kuzuru Washington wiki ijayo.
Hata hivyo, hakuthibitisha kama Machado atapewa nafasi ya uongozi, akisema huenda “akashiriki kwa namna fulani.”
katika hatua ingine, rais huyo amegusia maandamano yanayoendelea Iran, akisema anaunga mkono waandamanaji na kuonya kuwa Marekani inaweza kuingilia kati endapo ghasia zitaongezeka.
Kwa upande wa Greenland, wananchi wa eneo hilo wameeleza wasiwasi wao. Akizungumza na BBC mjini Nuuk, baadhi yao walisema wanataka kuachwa waamue mustakabali wao bila vitisho vya mataifa makubwa.
