Asema ndio sababu za kumteua Profesa Kabudi kuwa Ofisi ya Rais Ikulu
Na Said Mwishehe,Michuzi TVRAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema ameteua aliyekuwa Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango kuwa Mshauri wake katika uchumi na miradi na aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa mshauri wake katika mambo ya jamii.
Hivyo amesema kutokana na kuwa na washauri hao katika ofisi yake ndio maana ameamua kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kumteua aliyekuwa Waziri wa Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amemteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Kazi Maalum
Akizungumza leo Januari 10,2026 Ikulu Dar es Salaam katika hafla ya kuwapongeza wanamichezo mbalimbali wakiwemo timu ya Taifa Stars iliyofanikiwa kuingia 16 Bora katika michuano ya AFCON ,Rais Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea sababu ya kumteua Profesa Kabudi kuwa Ikulu.
“Pamoja na kwamba leo ni siku ya kuwapongeza wana michezo waliofanya vizuri kama vijana wangu wa Taifa Stars lakini pia shughuli hii imekuwa wakati maalum kumuaga Profesa Kabudi kutoka kwenye michezo na kuja kwangu Ikulu.
“Imekuwa mapema kubadilisha lakini kwasababu kuendana na siasa za dunia zinavyokwenda ambazo zinajicho chanya kwa Tanzania na nyingine jicho hasi kwa Tanzania.
“Pale Ikulu nahitaji akili iliyopevuka yenye maarifa mapana , uzoefu mkubwa na mtu ambaye yuko vizuri kujieleza na anaweza kulieleza jambo likaeleweka hivyo nimepiga picha serikalini kwangu kote nikasema Profesa Kabudi atanifaa
“Lakini jingine ni kwamba punde hivi nimeteua washauri wa Rais.Nimemteua aliyekuwa Makamu wa Rais kuwa mshauri wa uchumi na miradi na nimemteua aliyekuwa Waziri Mkuu atakuwa ananishauri mambo ya jamii.
“Sasa vile vichwa viwili vikubwa vinahitaji mtu aliyetulia mtulivu anayeweza kwenda nao,hawa watoto wangu wanaweza kujijibia tu ikaja kesi lakini Profesa Kabudi anaweza kwenda nao.
“Kwahiyo hiyo ndio sababu nimchukue Profesa Kabudi Ikulu aje anisaidie kazi lakini nikajipa moyo Mwana FA (Hamis Mwinjuma)na Makonda (Paul Makonda)wanaweza kuindesha Wizara ya Michezo vizuri kwasababu ni Wizara ya vijana na wao ni vijana hivyo wataweza ni vijana kwa vijana wenzao
“Ningesema Makonda afanye kazi na washauri wangu wale watu wangesema mama anamjua vizuri Makonda ? Lakini Makonda kwa vijana wenzie yuko vizur sana na Mwana FA kwa wanamistari wenzie yuko vizuri sana,”amesema Rais Samia akitoa sababu za kumteua Profesa Kabudi kwenda Ikulu.