TRA yapiga hodi ikimtaka Mzamiru Simba

BAADA ya kuinasa saini ya Denis Nkane kutoka Yanga, TRA United imehamia Simba ikiwinda saini ya mkongwe Mzamiru Yassin ili kuongeza nguvu eneo la kiungo.

TRA United inaendelea kuboresha kikosi ili kurudisha ushindani baada ya kuanza vibaya msimu huku ikipambana  kuendelea kubaki Ligi Kuu Bara.

Chanzo cha kuaminika kutoka TRA United kimeliambia Mwanaspoti kuwa ipo kwenye hatua nzuri kukamilisha usajili wa kiungo huyo ambaye amebakiza miezi sita kumaliza mkataba wake Simba.

“Ni kweli tunafanya usajili kutokana na mahitaji katika ripoti ya benchi la ufundi ambayo imeonyesha upungufu eneo la kiungo mkabaji, hivyo pendekezo bora lilikuwa kwa Mzamiru kutokana na uzoefu wake,” kilisema chanzo.

“Mchakato wa kukamilisha usajili wake unaenda vizuri na makubaliano ni kumsainisha miezi sita, na kipengele cha kumuongeza endapo atafanya vizuri katika miezi hiyo ya kumaliza msimu.”

Chanzo hicho kilisema timu hiyo ina imani kubwa na mchezaji huyo, ikiamini kama itakamilisha usajili wake, basi atakuwa chachu ya kuwa bora, na timu shindani kwenye mechi zilizobaki.

“Hatujawa na mwanzo mzuri, hilo halifanyi tukashindwa kuendana na kasi ya ligi msimu huu. Baada ya kuona tumetatizika mechi za kwanza tumebaini upungufu na kuufanyia kazi.”