Dar es Salaam. Wakati mawakili wa mtengeneza maudhui mtandaoni, Clemence Mwandambo, wakifungua shauri Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya, kuomba amri afikishwe mahakamani, tayari amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Temeke na kuachiwa kwa dhamana.
Mwandambo, mwalimu wa Shule ya Awali ya St. Clemence, amekuwa maarufu mitandaoni kutokana na maudhui yake yenye kibwagizo: “Nachoka baba yenu Clemence Mwandambo.”
Alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 29, 2025. Jana Januari 9, 2026 mawakili wake, Hekima Mwasipu na Phillip Mwakilima, walifungua shauri kuomba afikishwe mahakamani (Harbeas Corpus).
Wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mbeya, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Mbeya Mjini, Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (OCS) Mbeya Mjini na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kupitia hati ya dharura, mawakili hao walieleza mwombaji yuko kizuizini kinyume cha sheria na kwamba, wajibu maombi walikataa kuwaruhusu ndugu, marafiki na wakili wake kumuona.
Hatua hiyo walieleza inaathiri haki zake kikatiba na kukiuka utawala wa sheria.
“Hali hii inahitaji uingiliaji wa haraka wa mahakama ili kuokoa haki za kikatiba za mwombaji,” walieleza mawakili wa mwombaji.
Waliomba wakati wa usikilizwaji wa upande mmoja, mahakama iridhie kutoa wito wa haraka ili mwombaji afikishwe mahakamani. Katika usikilizwaji wa pande zote, waliomba mahakama iamuru mwombaji aachiwe kutoka kizuizi kisicho halali na wajibu maombi wafike mbele ya mahakama wajieleze kwa nini mwombaji amezuiwa kinyume cha sheria.
Pia, wajibu maombi wazuiwe kumshikilia mwombaji kinyume cha sheria kwa muda mrefu kinyume cha sheria.
Maombi hayo yaliungwa mkono na kiapo cha wakili Mwakilima, aliyeeleza mwombaji ni Mtanzania, mwanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania na mwalimu wa Shule ya Awali ya St. Clemence mkoani Mbeya.
Alidai katika kiapo kuwa Mwandambo kupitia mitandao ya kijamii ameonyesha uzalendo na mapenzi makubwa kwa Taifa kwa kufichua maovu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kama mkosoaji wa jamii akitumia kauli: “Nachoka mimi mzee wenu Mwandambo.”
Novemba 2025, Mwandambo alikamatwa na OCD Mbeya Mjini akituhumiwa kusambaza na kueneza taarifa za uongo, akaachiwa kwa dhamana ya polisi, akaamriwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya.
Anadai Desemba 29, 2025, aliripoti katika kituo hicho na tangu siku hiyo wajibu maombi waliamua kumweka kizuizini hadi wakati anatoa kiapo hicho, alikuwa anazuiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya.
“Nilipoomba kwa mjibu maombi wa pili (RPC), wa tatu (OCD) na wa nne (OCS) kumwachia mwombaji kwa dhamana ya polisi au kumfikisha mahakamani iwapo kuna makosa aliyotenda, walinieleza mteja wangu ni mgumu, mkaidi na haelewi wala hatii maagizo ya polisi,” alieleza wakili Mwakilima.
Alidai siku nyingine alipotaka kumuona mteja wake, wajibu maombi walimweleza wanatekeleza maelekezo ya IGP, hivyo ni lazima wapate kibali chake ili kumuona.
Alidai jitihada kuwezesha mteja wake kuachiwa kwa dhamana au kuweka huru ziligonga mwamba, akaendelea kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.
Hata hivyo, wakati mawakili wakipambana Mahakama Kuu Mbeya, Mwandambo alifikishwa Mahakama ya Wilaya Temeke, Dar es Salaam, Januari 9, 2026 bila mawakili wala ndugu zake kuwa na taarifa.
Akizungumza na Mwananchi, wakili Mwasipu amesema tangu Desemba 29, 2025 leo Januari 10, 2026 ndipo wamepata taarifa kuwa mteja wao alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Temeke, Dar es Salaam jana Januari 9, Jamhuri ikaomba akwekwe chini ya uangalizi.
Ameeleza baada ya mahakama kusikiliza upande wa Jamhuri ili kwa Mwandambo kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja, kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi aripoti Polisi Mbeya ndani ya mwaka mmoja kuanzia Januari 9, pamoja na kutoa akaunti zake zote za mitandao ya kijamii kwa Jeshi la Polisi.
“Baada ya kutoka mahakamani akapelekwa Kituo cha Polisi Chang’ombe na leo saa 6:00 mchana ndugu wakapigiwa simu ili wakamdhamini,” amesema Mwasipu.
