Unguja. Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa ya lazima ili kurejesha na kujenga heshima ya Mzanzibari, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa mpaka sasa.
Dk Shein ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Januari 10, 2026, wakati akifungua barabara ya kilometa 13.2 kutoka Kitogani hadi Paje, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kabla ya Mapinduzi, zilikuwapo baadhi ya barabara lakini hazikuwa na hadhi wala ubora, kwa kuwa wakoloni walizingatia zaidi maslahi yao binafsi bila kujali utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Vipaumbele vyao vililenga watawala wenyewe. Usafiri haukuwa na tija; wakati mwingine mtu alikuwa na hiari ya kutembea kwa miguu badala ya kutumia usafiri kutokana na miundombinu mibovu,” amesema Dk Shein.
Amesema wakati wa ukoloni, maendeleo yalikuwa hayana mwelekeo mzuri na miundombinu iliyojengwa ililenga zaidi maslahi ya wakoloni, huku barabara nyingi zikielekezwa kwenye mashamba yao pekee.
“Leo tumefika hatua ambayo karibu kila barabara imejengwa. Ndiyo maana ilikuwa lazima Mapinduzi yafanyike ili kurejesha heshima yetu sisi ni wenye nchi, kwa kuwa hatukuthaminika. Ilibidi tupange mambo yetu wenyewe,” amesema.
Kiongozi huyo mstaafu amesema kwa sasa heshima ya Zanzibar imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa miundombinu ya kisasa na yenye ubora, hali inayovutia wageni wengi kutembelea visiwa hivyo.
Amefafanua kuwa maendeleo hayo yamelenga kukuza utalii ambao umeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kipindi cha Mapinduzi, kulikuwa na hoteli mbili pekee na sasa ziko zaidi ya 400.
Dk Shein amesema miundombinu ya barabara siyo tu inachochea ukuaji wa utalii, bali pia inaboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha biashara kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka eneo moja kwenda jingine.
“Biashara inashamiri, mazao yanapata soko na hivyo kuchochea uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi na madereva kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo ili idumu kwa muda mrefu, akibainisha kuwa serikali hutumia gharama kubwa katika ujenzi wa miundombinu yake.
“Nilipokuwa serikalini najua gharama za ujenzi wa barabara zilivyo. Kilometa moja ya lami ni fedha nyingi sana, hivyo tuna kila sababu ya kuhakikisha miundombinu hii inatunzwa,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuheshimu maeneo yanayotengwa na serikali kama hifadhi za barabara, kwa kuepuka kuyavamia kwa shughuli za ujenzi au biashara, kisha kudai fidia pale serikali inapohitaji kuyaendeleza.
“Unakuta alama inaonyesha eneo hili ni hifadhi ya barabara, mtu anajenga. Serikali ikitaka kupanua miundombinu, anataka kulipwa fidia. Uliitwa?” amehoji Dk Shein, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu alama rasmi.
Akitoa taarifa za kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakari, amesema barabara ya Kitogani–Paje yenye urefu wa kilometa 13.2, imejengwa kwa gharama ya Sh26.7 bilioni.
Amesema barabara hiyo ni miongoni mwa barabara za vijijini zenye jumla ya urefu wa kilometa 277.7, ambazo mkataba wake ulisainiwa Juni 2023 kwa gharama ya Dola za Marekani 308 milioni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa amesema katika mkoa huo, jumla ya miradi 23 ya maendeleo imefunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi, ikiwemo miradi ya miundombinu.
Amesema ujenzi wa barabara hizo unalenga kuimarisha uwekezaji unaoendelea kufanyika katika mkoa huo.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kabla ya Mapinduzi kulikuwapo barabara zenye urefu usiozidi kilometa 10, huku kwa sasa Zanzibar ikiwa na mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,344 katika visiwa vya Unguja na Pemba.
