Rais Samia Awateua Mpango na Majaliwa Kuwa Washauri Wake – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko makubwa ya kimkakati katika safu ya washauri wake, akiwateua aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, na aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa Washauri wa Rais.

Akizungumza leo, Januari 10, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwapongeza wanamichezo waliofanya vizuri kimataifa, Rais Samia amefafanua kuwa Dkt. Mpango atakuwa mshauri wake katika masuala ya uchumi na miradi, wakati Kassim Majaliwa atakuwa mshauri katika masuala ya kijamii.

Rais amesema amemhamisha Profesa Palamagamba Kabudi kutoka Wizara ya Michezo na kumteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum), ili kuratibu na kufanya kazi kwa karibu na washauri hao wapya.

“Pale Ikulu nahitaji akili iliyopevuka yenye maarifa mapana, yenye uzoefu mkubwa na mtu ambaye yuko vizuri kwenye kujieleza na kueleza jambo likaeleweka. Nimepiga picha serikalini kwangu kote nikasema Profesa Kabudi atanifaa”, amesema Rais Samia akielezea sababu za kumrejesha Prof. Kabudi Ikulu.

Rais Samia amebainisha kuwa siasa za dunia kwa sasa zinaitazama Tanzania kwa macho mawili- chanya na hasi, hivyo anahitaji safu imara ya washauri wenye uzoefu mkubwa. Ameongeza kuwa Profesa Kabudi atakuwa kiungo muhimu kati ya Rais na washauri hao wawili (Mpango na Majaliwa), akimtaja Profesa kama mtu mtulivu anayeweza “kudeal” na vichwa hivyo vikubwa vya uongozi.