Mtunisia Azam anukia Irak | Mwanaspoti

KLABU ya Azam huenda ikaachana na winga Mtunisia Baraket Hmidi, baada ya mchezaji huyo kushindwa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkongomani Florent Ibenge tangu asajiliwe.

Nyota huyo aliyejiunga rasmi na Azam, Agosti 16, 2025, akitokea CS Sfaxien ya kwao Tunisia, inadaiwa ataondolewa katika dirisha hili dogo la Januari, ambapo hadi sasa tayari mazungumzo yanaenda vizuri kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya.

Taarifa zinaeleza miongoni mwa klabu inayowania saini yake katika dirisha hili dogo la usajili ni Diyala SC inayoshiriki Ligi Kuu Irak, ambapo mabosi wa kikosi hicho wamefungua mazungumzo na Azam kwa ajili ya kupata huduma ya winga huyo.

Chanzo hicho kinaeleza makubaliano yaliyopo ni ya kwenda timu nyingine kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, kwani mkataba wake na Azam unaisha Juni 30, 2027, ingawa atarejeshwa tena kikosini ikiwa tu atakuwa na kiwango cha kushindania nafasi.

Tangu nyota huyo ajiunge na Azam, ameshindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, nyuma ya wazawa, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Idd Seleman ‘Nado’, jambo linalochangia zaidi kutolewa ili kupisha wachezaji wengine.

Nyota huyo tangu ajiunge na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam msimu huu, amechangia bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Mbeya City, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Septemba 24, 2025.