Damaro atibua hesabu za Pedro Yanga

ILE kadi nyekundu aliyoonyeshwa kiungo wa Yanga, Mohamed Damaro katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 dhidi Singida Black Stars, imemuumiza kichwa kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves.

Damaro alionyeshwa kadi hiyo baada ya kumchezea rafu kiungo wa Singida, Morice Chukwu ambaye naye aliadhibiwa kwa kadi hiyo.

Tukio hilo lilitokea dakika ya 85, ambapo katika kuwania mpira wa juu, Damaro alionekana kumpiga kiwiko Chukwu ambaye baada ya kuanguka, akaamka haraka na kwenda kumsukuma mwenzake.

DAMA 01

Mwamuzi Rashid Farahan akaanza kumuonyesha kadi ya njano Damaro ambayo ilikuwa ya pili baada ya kwanza kuonyeshwa dakika ya 33, hivyo ikafuatia nyekundu, huku Chukwu akionyeshwa nyekundu moja kwa moja.

Akizungumzia kadi hiyo ambayo inamfanya Damaro kukosa mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam itakayochezwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, Pedro amesema kwanza hakufurahishwa na tukio lenyewe.

“Ndiyo, kwa hakika. Sifurahishwi na hali ilivyo sasa, lakini Damaro alitakiwa kuendelea kuwa makini na kuweka akili kwenye mchezo. Tangu tulipokuwa na tukio la kadi ya njano, ilitulazimu kuwa tayari kucheza akiwa na kadi ya njano kwa sababu tunataka zaidi kutoka kwa kila mchezaji.

DAMA 02

“Bila shaka, tunahitaji kusimamia hilo vizuri. Najua, lakini pia nataka kuunda mazingira hayo na kushughulikia hali hiyo kwamba tunapokuwa na kadi ya njano, inabidi kuwa waangalifu, lakini bado kucheza kwa kiwango kilekile.

“Ndiyo, kuwa makini. Lakini Singida wanamfahamu vizuri sana. Wakawa wanamchokoza pia. Mwishowe, hali kama hiyo inatokea. Najua vijana wale ni marafiki, lakini ndio hivyo soka lilivyo.

“Nimepoteza wachezaji wengi kuelekea fainali. Katika mechi ya kwanza nilipata majeruhi. Pia wapo waliokuwa AFCON, na Dube amewasili.

DAMA 03

“Nilimpa dakika chache za kucheza. Ni muhimu pia kwa yeye kurudi uwanjani na kucheza na wenzake. Kwa hiyo, tunapaswa kukabiliana na changamoto hizo. Na kila wakati ni fursa kwa mwingine.

“Tunahitaji kufikiria kwa mtazamo chanya kama kawaida. Ndiyo, ni kurudia jambo lile lile, lakini si hali ya kuniangusha. Tusikate tamaa, tusimame na tukabiliane na hali, na tuunde fursa mpya,” amesema Pedro.