Abate Temu: Kuweni Majasiri kusema ukweli, kupigania haki

Dar es Salaam. Abate wa Abasia ya Ndanda wa Kanisa Katoliki, Christian Temu amesema Wakristo wanapaswa kutambua kuwa woga si jambo la kuchagua, bali wanawajibika kuwa wajasiri, kupenda kusema na kusimamia ukweli na kuzungumzia masuala ya haki bila kuogopa.

Abate Temu amesema hayo ni kwa sababu haki na amani ni matunda ya Kimungu yasiyotengenezwa na mwanadamu yeyote.

Ameyasema hayo leo Jumamosi, Januari 10, 2026, wakati wa adhimisho la misa ya kufunga Mwaka wa Jubilei Kuu 2025, iliyofanyika katika Kituo cha Hija Pugu, jijini Dar es Salaam.

Amesema muumini anayemwamini Mungu anapaswa kuwa na ujasiri wa kusema ukweli, kutaja haki ya mtu kwa jina lake Mungu na kusimamia amani katika familia, kigango, jumuiya na maeneo yote ya maisha.
“Wapo watu wenye mapenzi mema ambao licha ya msukumo uliopo katika jamii, wanasimama katika ukweli, wanatetea haki na kusimamia amani ya kweli. Hivyo niwaombe na sisi tutazame mbele kwa matumaini. Usiogope hata kama unapita katika maji mengi au uvuli wa mauti, mtambue kuwa Yesu yupo,” amesema kiongozi huyo.

Amesema katika wakati wa sasa, kila mtu anakabiliwa na changamoto zake, akitolea mfano watu wanaougua saratani, kisukari na shinikizo la damu.

“Hili linaonyesha kuwa hakuna anayejua hali ya afya ya mwenzake. Kila mtu ana mahangaiko yake, lakini ni vyema Wakristo kutembea wakitambua kuwa Mungu yupo na anatembea na kila mmoja, hivyo msiogope,” amesisitiza Abate Temu.

Ameongeza kuwa imani inaweza kuwa hai katika kutenda na kusema, lakini katika kuyasimamia hayo si kila jambo litakuwa rahisi.

Kwa msingi huo, amewataka waumini kuendelea kumshukuru Mungu kwa kutembea nao katika kipindi chote cha mwaka, akibainisha kuwa kwa pamoja wanakubaliana kuwa mwaka 2025 haukuwa mwepesi.

“Hata hivyo tusisahau kuwa Mungu ni mwaminifu. Yupo na tuendelee kumtumainia katika hija ya safari yetu kama wanakanisa na Watanzania,” amesema.

Akizungumzia adhimisho la misa hiyo, Abate Temu amesema ilikuwa maalumu kwa ajili ya kusherehekea wakati wa sasa kwa furaha, akieleza kuwa safari ya maisha ni ndefu na ina jana, leo na kesho.

“Pamoja na hofu na mashaka tuliyonayo, bado tunapumua na tumeweza kuwa hapa, tukakutana na viongozi wa dini. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo,” amesema.

Amesema imani waliyonayo waumini ni urithi wa thamani kubwa walioupokea kutoka kwa mabibi na mababu waliotangulia.

“Imani haina bei. Si bure, lakini hata mtu akiambiwa akane imani yake kwa Sh10 bilioni, bado si thamani yake. Tuijue imani yetu, tuipende, tuihifadhi na kuona fahari kuwa Wakristo Wakatoliki. Ili kuitetea imani inakupasa kuwa jasiri,” ameongeza.

Akitoa mahubiri katika misa hiyo, Abate Temu amesema amefurahishwa na nidhamu na maandalizi ya waumini waliofika kituoni, akibainisha kuwa hakuna aliyevaa kijora bali wote walikuwa nadhifu, wakisali na wengine kuungama.
“Tulipokuwa tunakuja asubuhi tuliona umati mkubwa wa watu waliovaa vizuri, wenye furaha, wengine wakiwa wanaungama na wengine wakisali. Nikatazama kama kuna aliyevaa kijora au dera, lakini hakuna. Kama tunavyosoma katika kitabu cha Ufunuo, tunaambiwa hawa ni wale walioosha mavazi yao katika damu ya mwanakondoo,” amesema.

Ingawa hakufafanua, ujumbe huo wa Abate Temu ulilenga tukio la hivi karibuni la watu walioenda Ubalozi wa Vatican jijini Dar es Salaam wakijifanya Wakatoliki, wakidai kupeleka malalamiko dhidi ya viongozi wao.

Watu hao walikosolewa mitandaoni kuwa mavazi yao ya vijora na madera, ambayo yalithibitisha si Wakatoliki, bali walikusanywa kutimiza malengo fulani.

Suala hilo pia limezungumziwa na Abate Pambo Mkorwe kuwa Kanisa Katoliki lina urithi wa imani linaojivunia, hususan katika masuala ya liturujia, akisisitiza kuwa namna Mkatoliki anavyoimba na kusali, hujitambulisha wazi bila shaka yoyote.

Amesema urithi huo unapaswa kudumishwa na kuenziwa, akieleza kuwa nyimbo na sala za Kanisa Katoliki zina utambulisho wake maalumu.

“Wimbo wa Kikatoliki unamtambulisha moja kwa moja huyu ni Mkatoliki. Huwezi kuimba chochote tu; sisi tunayo ya kwetu. Hata namna Mkatoliki anavyosali, anavyoanza na kumalizia sala, unajua wazi huyu ni Mkatoliki, haanzi kwa kutaja chochote,” amesema.

Abate Mkorwe ameongeza kuwa miongoni mwa urithi muhimu wa Kanisa Katoliki ni nidhamu, “nikiwa nyumbani nahesabu nguruwe ni tofauti na ninapoenda katika ofisi ya Mheshimiwa Baba Askofu Mkuu; kuna namna yake na kuna mavazi yake.”

Aidha, amewahimiza waumini kuwaombea viongozi wao wa kiroho, akionya kuwa adui huwalenga viongozi ili kuwavuruga waumini.

“Shetani hana adabu, na anajua akimpiga mchungaji kondoo watatawanyika. Usikubali Mkatoliki kufanywa kituko au kinyago kwa kuwekwa kinywani maneno ya kukejeli Kanisa lako, wajibu wako ni kulilinda Kanisa,” amesema.