Tulia agusa wanafunzi 3,000 waishio mazingira magumu

Mbeya. Mbunge wa Uyole Mkoa wa Mbeya, Dk Tulia Ackson ametoa mahitaji mbalimbali zikiwepo sare za shule kwa wanafunzi 3,000,waishio mazingira magumu katika kata 13 jimboni kwake.

Hatua hiyo imetajwa ni kuwezesha kundi hilo kupata elimu bora kama jamii nyingine na kuweka bayana mikakati yake ya kuwezesha sekta ya elimu hususani kutoa kompyuta kwa walimu.

Dk Tulia ambaye ni Spika wa Bunge Mstaafu, ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Januari 10, 2026, kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Hasanga katika hafla fupi ya kukabiliana mahitaji kwa wanafunzi 3,000, kuanzia elimu ya awali hadi darasa la saba.

“Kimsingi sare tunazotoa leo zina ubora mzuri, lakini nafanya hivi kwa lengo la kusaidia kundi hilo kupata elimu bora kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ambayo inatenga fedha nyingi kuboresha miundombinu ya kujifunza na kujifunzia mashuleni, “amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Tulia ameweka bayana mikakati ya kuanzisha programu maalumu ya kugawa kompyuta kwa walimu mashuleni kwa lengo la kuboresha taaluma ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Amesema ni mipango yake kuhakikisha sekta ya elimu inafanya vizuri na hakuna mtoto anabaki nyumbani kwa kukosa mahitaji mbalimbali ya shuleni.

Wakati huo huo amewataka wazazi kusimamia familia katika suala zima la upatikanaji wa elimu bora na kuwa mabalozi kwa wale wanaokwama kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali.

Naye, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema kupitia programu ya Tulia Trust Education zaidi ya watoto 200,waishio mazingira magumu wamepata fursa ya kuendelea kielimu ndani na nje ya nchi.

Mwakanolo amesema kupitia mpango huo wamefanya tathimini ya awali na kubaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya wanafunzi wenye mahitaji kabla ya muhula wa masomo kuanza ili kutimiza ndoto za kupata elimu.

“Tulifanya tathimini kwa kushirikiana na viongozi husika kubaini kundi lenye changamoto kubwa ya mahitaji na kufanya mahitaji kwa kushirikiana na mafundi kwenye Kata husika,”amesema.

Mwakanolo amesema mchakato huo ulianza mwaka 2025/2026, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kurejesha tabasamu kwa watoto waishio mazingira magumu hususani familia wanazotoka.

Mwakanolo amemuomba Dk Tulia, kuona namna ya kuwepo mpango mkakati wa kusaidia familia za makundi hayo ambao wamejikita katika kilimo au kufanya vibarua kwa ajili ya kupata fedha za mahitaji.

“Asilimia kubwa familia hizo zinategemea fedha za mahitaji kwa kufanya vibarua vya kulima ni vyema kuona namna bora kuziwezesha ili kuboresha shughuli hizo na kujikwamua kiuchumi,”amesema.

Mmoja wa wanufaika Sekela Alex (20), amesema Dk Tulia amewafuta machozi kutokana ugumu wa maisha na wengi wao kuwa njia panda katika kipindi hiki cha maandalizi ya watoto kwenda Shule.

“Nilikuwa sina mbele wala nyuma nina watoto watatu mwingine mmoja wa marehemu mdogo, sasa nimepata matumaini yaliyo potea kwa kukabidhiwa mahitaji.

Diwani Kata ya Itezi Jimbo la Uyole, Angetile Kapolesya amesema kimsingi wanapaswa kumuombea Dk Tulia Mungu amtunze kwa matendo makubwa ya kugusa jamii ya wahitaji.