Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya siasa na sheria nchini wamebainisha mzigo mzito wa majukumu unaomsubiri Waziri mteule wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, ikiwemo upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa, kukomesha utekaji na kujenga uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Katambi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo Januari 8, 2026, akichukua nafasi ya George Simbachawene ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Uteuzi wa mbunge huyo wa Shinyanga Mjini, umekuja katika kipindi ambacho baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, hususani Jeshi la Polisi, ambalo utendaji umekuwa ukikosolewa, huku mtangulizi wake akiwa ameweka bayana mikakati ya kulifanyia mageuzi jeshi hilo.
Akiwa anasubiri kuapishwa Januari 13, 2026 kuanza rasmi majukumu hayo mapya, Katambi anakabiliwa na kibarua kigumu katika kusimamia utendaji wa jeshi hilo na taasisi nyingine zilizo ndani ya wizara yake, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya sheria na siasa.
Akizungumzia yanayomkabili Waziri huyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema wizara hii inahusiana na usalama wa raia na kwamba kwa muda mrefu imekuwa na changamoto nyingi kama vile ukamataji mbaya.
“Hata Rais aliamua kuunda kamati ya haki jinai iliyotoa mapendekezo ya kuliboresha (Jeshi la Polisi). Changamoto kubwa kwake, anatakiwa kulifanyia mabadiliko jeshi hilo, jambo ambalo si rahisi kwani mpaka liridhiwe na Rais na viongozi wengine.
“Kazi nyingine ni kurejesha imani ya wanachi kwa Jeshi la Polisi na kujenga uadilifu kwa jeshi hilo katika utendaji wake. Mbali na mtihani huo, Jeshi la Magereza nalo limekuwa na changamoto nyingi ambazo anapaswa kulitazama na kuzishughulikia,” amesema.
Mbali na hilo, amesema Katambi ana mtihani wa kushughulikia kero ya vitambulisho vya Taifa (Nida), ambayo imekuwa ikipigiwa kelele nyingi na wananchi, haya ni mambo ambayo anatakiwa kuyashughulikia ili kuweka vizuri wizara hiyo.
Kwa upande wake, wakili Dk Onesmo Kyauke amesema kipaumbele kikubwa kwa Katambi kinapaswa kuwa namna ya kukamata, kushikilia na kuchunguza watuhumiwa kwa mujibu wa sheria, akitaja kuwa hilo ni jambo linalopaswa kushughulikiwa mara moja.
“Kukamatwa lazima kuwe kwa msingi wa tuhuma halali, kwa kufuata taratibu za kisheria, heshima na utu wa mtu, na bila matumizi mabaya ya mamlaka,” amesema.
Amesema anapaswa kuliekeza Jeshi la Polisi na vyombo vya dola kuwa kukamata si adhabu, bali ni hatua ya kisheria inayolenga uchunguzi na kwamba haki ya mtuhumiwa ikiwemo kupewa sababu za kukamatwa, kuwasilishwa mahakamani kwa wakati na kupata dhamana pale inapostahili, lazima ilindwe.
“Pia, anatakiwa kuanzisha mafunzo endelevu kwa Polisi kuhusu haki jinai, ushahidi na taratibu za kukamata na kuhoji watuhumiwa. Polisi mwenye maarifa ya kisheria hupunguza makosa yanayosababisha kesi kuanguka mahakamani,” ameongeza.
Dk Kyauke amesema jambo jingine linalomsubiri Katambi ni kurudisha uhusiano mwema kati ya Polisi na raia, na kuangalia maslahi ya Polisi hasa mishahara mizuri na kuboresha makazi yao ili utendaji wao uwe mzuri.
Wakili wa kujitegemea, Faraji Mangula amesema changamoto zinazomsubiri waziri huyo ni kuhakikisha usalama wa raia hasa suala la utekaji wa watu, suala alilolikomalia Simbachawene akitaka mabadiliko ya mifumo ya Polisi.
Amesema Katambi anatakiwa aanzie alipoishia Simbachawene kwa kuhakikisha usalama wa raia unalindwa na kuzuia ukamataji holela wa watu.
“Ukamataji uwe wa kisheria, askari wajitambulishe kwenye serikali ya mtaa kabla ya kumkamata mtu na watuhumiwa wasipewe bughuza.
“Pia, asimamie magari ya askari wanapokwenda kutekeleza majukumu yao watumie magari yenye namba rasmi ili kuondoa taharuki kwenye jamii,” amesema.
Msimamo wake akiwa upinzani
Punde baada ya uteuzi wake katika wizara hiyo, baadhi ya video zimepata umaarufu mkubwa mitandaoni zikikumbushia matamko yake aliyowahi kuyatoa kwa vyombo vya habari wakati akizungumzia mwenendo wa Jeshi la Polisi wa ukamataji wa viongozi wa Chadema na watu wengine bila kufuata taratibu za kisheria.
Katika nukuu hizo, Katambi alikuwa akisisitiza kuhusu weledi na kuheshimu sheria kwa Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yake, akikosoa kile alichokuwa akikiita ‘maelekezo kutoka juu’ ambacho alidai kilikuwa kikitumia na waliokuwa wakiwakamata viongozi wa Chadema.
Alikuwa akikosoa vitendo hivyo na kuwataka maofisa wa polisi wanaotenda hayo kwa madai ya maagizo kutoka juu kuthibitisha maagizo hayo kwa maandishi kutoka kwa mamlaka inayotoa maagizo hayo batili.
Katambi alikuwa akionya kuwa kufanya hivyo ni kuichafua serikalki na kumchafua rais, akisisitiza kuwa sheria haitambui uajibikaji wa pamoja na kuwatahadharisha askari kuwa kufanya kosa hilo kunaeza kuwaajibisha binafsi bila kuigusa serikali kwa ujumla.
Katika kauli nyingine iliyonukuliwa na kusambaa sana mitandaoni, Katambi alisisitiza juu ya suala la mamlaka na heshima ya sheria akikemea viutenbdo vya jeshi la polisi kukamata viongozi wa upinzani akihoaji kuwa upinzani si kosa.
Katambi alisema Jeshi la polisi ni chombo cha kisheria na kiupelelezi kinachopaswa kuaminika katika jamii badala ya kulaumiwa kwa kukamata viongozi wa upinzani kikandamizaji hali aliyodai inadhalilisha serikali.
Katambi aliibuka nyakati kadhaa akimkosoa moja kwa moja aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Mwigulu Nchemba, ambaye sasa ni Waziri Mkuu wa Tanzania, akimtuhumu kushindwa kusimamia vyema wizara hiyo na Jeshi la Polisi lililokuwa chini yake akitaja hatua zilizofaa kuchukuliwa.
Katika hatua hiyo, Katambi alisisitiza kuwa vitendo viovu vya jeshi la polisi vinastahili kukemewa na waziri mwenye dhamana hiyo na kuvikalia kimya na kuviacha kuendelea huku vikishafua taswira ya Serikali na Rais kwa wananchi lakini yeye alikuwa amelala uzingizi.
Pamoja na kauli hizo, wachambuzi wa habari na siasa wamekuwa na maoni tofauti iwapo kwa sasa ataweza kusimamia mageuzi hayo, licha ya kumtaja kama mwenye msimamo na maono ya wazi kuhusu maboresho hayo, kabla ya kujiunga na chama tawala
“Katambi anao mtihani mgumu kutimiza matamanio ya Watanzania hasa kwa sababu matatizo ya wizara hiyo anayajua na yeye ndiye aliyekuwa akiyakemea alipokuwa Chadema,” amesema Wakili Aloyce Komba katika mazungumzo na Mwananchi.
Komba amesisitiza kwamba: “Hukuna Waziri wa Mambo ya ndani tangu mwaka 2000, aliyedumu zaidi ya miaka miwili. Kwa nini? Katambi asimamie haki aliyoililia akiwa Chadema. Swali ni ataweza na atajitofautishaje na Simbachawene?”
Kwa upande wake, Mwanahabari nguli, Absolom Kibanda anauona mtihani wa kwanza kwa Katambi ni msimamo wake na maono yake, akisema licha ya kuwa ndio msimamo wa wengi, anaonekana kufanana kimaono na mtangulizi wake, Simbachawene ambaye ametenguliwa na kuacha maswali.
“Katambi ni mtu mwenye msimamo unaofanana na aliokuwa nao mtangulizi wake, Simbachawene, akiwa katika wizara hiyo. Hii inatoa tahadhari kuwa ikiwa Simbachawene aliondolewa kwa kauli zake na msimamo huo, basi Katambi anapaswa kuwa makini,” amesema.
Akimtazama kwa jicho hilo, Dk Conrad Masabo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, anasema mtihani mwingine kwa Katambi, utakuwa ni chama chake na malengo ya Serikali, ambavyo vinaweza kuathiri msimamo wake na maono yake ya awali.
“Kwa vyovyote vile hatajitofautisha na viongoizi wenzake ndani ya chama na mfumo wa Serikali, hayo ndiyo yataamua awe kiongozi wa namna gani, msimamo na maono yake ya wakati alipokuwa nje ya CCM yalitokana na chama na watu aliokuwa nao,” amesema.
Akiwa na mtazamo tofauti na huo, mchambuzi wa siasa nchini, Hamduny Marcel amesema Katambi ni chaguo sahihi kwa nafasi hiyo, akitaja sifa zake za kitaaluma na uzoefu wake katika nafasi alizopata kuhudumu awali, kuwa atafanya mageuzi makubwa katika wizara hiyo kuendana na matamanio ya walio wengi.
“Katambi ni kijana mzuri, ana elimu nzuri ya sheria na wizara hiyo aliyopewa ina mambo mengi sana. Ukiacha Jeshi la Polisi, ina mambo ya Uhamiaji na mengine mengi ambayo yanahitaji taaluma ya sheria. Pia, kwa uzoefu wake katika nafasi alizopita, anaweza kutatua vikwazo na kufanya mageuzi,” amesema.
