UONGOZI wa Simba uko katika hatua za mwisho za kumuongeza kwenye benchi la ufundi kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 19 ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Kristopher Charles Bergman, ili akaungane na Kocha Mkuu, Steven Robert Barker.
Barker, raia wa Afrika Kusini aliyetambulishwa kuiongoza timu hiyo Desemba 19, 2025, akichukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyeondoka Desemba 2, 2025, inaelezwa amempendekeza Bergman aongezwe kwenye benchi la ufundi la kikosi hicho msimu huu.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kocha huyo ameutaarifu uongozi wa Mamelodi nia yake ya kutaka kuondoka na tayari makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba yako katika hatua za mwisho ili ajiunge na Simba.
Bergman aliyezaliwa Januari 31, 1989 jijini Cape Town, Afrika Kusini, inaelezwa amepeleka maombi yake kwa uongozi wa Mamelodi ili wamruhusu kutafuta changamoto sehemu nyingine mpya, ambapo hadi sasa kila kitu kinaenda vizuri.
Kocha huyo enzi za uchezaji wake alicheza beki wa kulia, beki wa kati na kiungo katika timu mbalimbali za Santos FC Cape Town Youth ya vijana, Santos FC Cape Town, All Stars FC, Chippa United FC na Ubuntu Cape Town FC zote za Afrika Kusini.
Pia, Bergman aliwahi kuichezea Stellenbosch FC ya Afrika Kusini aliyojiunga nayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, akitokea Ubuntu Cape Town FC, ambapo kwa wakati huo alifanya kazi kwa ukaribu na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Steven Barker.
Taarifa zinaeleza, uhusiano mzuri wa kazi kati ya Barker na Bergman, unachochea zaidi kwa kocha huyo kutua Simba, ambapo kwa sasa kumebaki mambo machache ya kukamilisha dili hilo, ili mtaalamu huyo aongezwe tena kwenye benchi hilo la ufundi.
Ikiwa dili la Bergman litakamilika, ataungana kwenye benchi la ufundi la kikosi hicho cha Simba na Kocha, Steven Barker, Kocha wa Makipa, Mzambia Davies Phiri na Kocha wa mazoezi ya utimamu ya mwili (fitness Coach), Sibusiso Meshack Makhula.
Pia, Bergman atashirikiana na Kocha Msaidizi, Selemani Matola aliyehudumu nafasi hiyo tangu mwaka 2019, akitokea Polisi Tanzania, ambaye alidaiwa huenda angepigwa chini baada ya kuondoka Dimitar Pantev, ingawa upepo ulibadilika na kubakia.
