TRA yaeleza mikakati ya kudhibiti upotevu wa mapato

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda amesema wataendelea kupambana na watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji wa kodi kwa kudhibiti mianya inayotumika kukwepa kodi.

Juzi, akihitimisha kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/26 kilichofanyika kwa muda wa wiki moja jijini Arusha,  Mwenda amesema hawatawavumilia vitendo vyovyote vya ukwepaji wa kodi.

Amesema miongoni mwa hatua watakazochukua ni kuimarisha mipaka, kuzuia magendo na kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa jamii sambamba na elimu ya magendo.

Sambamba na kupambana na wakwepaji kodi, amesema wamejipanga kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya wakiwamo wafanyabiashara ambao bado hawajaingia katika mifumo ya kulipa kodi.

Amesema kazi ya kukusanya kodi ni ya watumishi wote na si maofisa kodi pekee, hivyo kila mtumishi wa TRA anapaswa kuhakikisha anatumia ubunifu, weledi na kuzingatia maadili ili kutimiza malengo ya TRA ya kukusanya Sh36.06trilioni katika Mwaka wa Fedha 2025/26.

“Na mimi ninatamani siku moja TRA iiwezeshe nchi yetu kuweza kujitegemea,” amesema Mwenda na kuongeza kuwa, ni matumaini yake kuiona TRA inakusanya kodi kwa ufanisi na hatimaye kulifanya Taifa kujitegemea kupitia kodi zake.

Akizungumza kuhusu mikakati ya ukusanyaji kwa Nusu ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/26 , Mwenda amesema TRA imejidhatiti kuhakikisha inaendelea kutumia mifumo katika ukusanyaji wa kodi huku akiutaja mfumo wa IDRAS ambao utaanza rasmi Februari 9, 2026.

Amesema TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu kama ilivyo jadi yake kwa kuwasikiliza walipakodi, kuwezesha biashara zao na kutatua changamoto zinazowakabili huku akiishukuru Serikali ya kwa kuipatia TRA watumishi wapya huku akitoa wito kwa viongozi kuwasimamia watumishi hao ili waweze kuleta tija katika utendaji wa majukumu yao.

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan amewataka watumishi wa TRA kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi, kutanua wigo wa walipakodi na kupambana na njia mbalimbali za ukwepaji wa kodi.

Amewapongeza watumishi wa TRA kwa kuendelea kufanya kazi na bidii hali iliyowawezesha kuvuka malengo kwa miezi 18 mfululizo huku ikiweka rekodi ya juu kabisa ya makusanyo kwa kukusanya Sh4.13 trilioni kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRA Moshi,  Jonathan Kabengwe amewapongeza wajumbe walioshiriki mkutano huo huku akiwataka kuzingatia yote waliyokubaliana katika mkutano huo ili TRA iendelee kuvuka malengo ya Makusanyo.

Aidha, amewapongeza watumishi wa TRA wanaotarajiwa kustaafu ndani ya mwaka huu wa 2026 huku akisema kuwa watumishi hao wameacha alama katika utendaji wao wa kazi.

Mkutano huo wa siku 5 wa kutathmini utendaji kazi wa TRA kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 umeshirikisha jumla ya washiriki 477 kutoka ofisi za TRA nchi nzima.