Anapa kuzalisha mazao mapya ya utalii

Arusha. Ikiwa zimepita siku chache tangu jarida la Kimataifa la  CNN Travel kutaja Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Anapa), miongoni mwa maeneo bora ya kusafiri mwaka 2026,Hifadhi hiyo imejipanga kuanzisha mazao mapya ya utalii.

Lengo la uanzishaji wa mazao mapya ya utalii ni kuongeza watalii wa nje na ndani ili kujionea vivutio hivyo ikiwemo Mlima Meru, Ziwa Momella na utalii wa kutazama twiga.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Januari 11,2026 na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Uhifadhi, Witness Shoo, wakati shughuli mbalimbali za utalii zikiendelea hifadhini humo ambapo amesema hiyo ni heshima kubwa kwa hifadhi hiyo na kuwa itawaongezea kupata watalii zaidi.

Amesema kuwa hifadhi hiyo yenye vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Meru, misitu minene, maporomoko ya maji na vivutio vingine na kuwa watazalisha mazao mapya ya utalii ili kuongeza watalii wa ndani na nje.

“Hivi karibuni Arusha ilitajwa kama sehemu nzuri ya kutembelea ikiwemo Hifadhi ya Arusha, kutokana na vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Meru, kreta ya Ngurdoto na maziwa ya Momella ambayo yanapambwa na ndege aina ya flamingo sambamba na Mto Ngarenanyuki wenye maji ya kahawia na ya kipekee,” amesema na kuongeza.

“Tuna misitu minene ambayo ina mbega weupe na weusi ambao unaweza kupiga nao picha kwa karibu lakini kufanya matembezi ya miguu, baisikeli na kupiga makasia ziwani,”

Mhifadhi huyo amesema kuwa wataanzisha mazao mapya ya utalii ili kuvutia utalii zaidi pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji ambapo waliwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa hizo kwa mujibu wa taratibu na sheria.

“Niwakaribishe kwenye hifadhi ya kipeke ambayo ina mlima, sehemu tambarare, maporomoko ya maji na vitu vingine. Kama nchi nyingine wameona ni sehemu bora kutembelea mwaka 2026,tunahamasisha watanzania kuendelea kutembelea vivutio vilivyopo nchini,” ameongeza

Mhifadhi huyo amesema katika kipindi cha mwaka 2024/25 hifadhi hiyo ilikuwa na ongezeko la wageni kutoka 60,000 hadi 72,000  na kuwa wanatarajia mwaka huu kupokea wageni zaidi ya 100,000.

Mmoja wa watalii, Suraji Navarante, amesema kati ya vitu vilivyomvutia hifadhini humo ni pamoja na mwonekano wa Mlima Meru, maporomoko ya maji pamoja na mazingira tulivu.

“Iwapo unataka kufanya safari nimeona hifadhi hii ni miongoni mwa  bora kwani kuna mazingira tulivu ambayo yanaweza kufanya safari yako iwe nzuri,” amesema.

Awali Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Buhohela amesema mbali na wageni wa nje, filamu ya The Royal Tour imeongeza hamasa ya Watanzania kutembelea Hifadhi mbalimbali hapa nchini.

“Filamu hiyo na Amazing Tanzania zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Tanzania nje pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani na  tunaendelea kuhamasisha zaidi ili tuongeze mapato,” amesema

Mmoja wa watalii kutoka mkoani Kilimanjaro, Gedion Swai amesema wao kupitia kikundi chao kwa mwaka huu wameamua kutembelea hifadhi huo ili kujionea vivutio vilivyomo.

“Tumeamua mwaka huu tusiingie kuona wageni wakija kwenye hifadhi zetu bali na sisi tuje kujionea vivutio vilivyopo hifadhini na kufurahia kwa pamoja badala ya kuishia mijini tu,” amesema

Ripoti iliyochapishwa Desemba 31,2025 na jarida hilo ilitaja hifadhi hiyo kama moja ya maeneo bora ya kusafiri kwa mwaka 2026.