Ujio teknolojia majiko ya umeme kuwagusa Watanzania hali ya chini

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikidhamiria Watanzania wanne kati ya watano watumie nishafi safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 wadau sekta hiyo wameonesha nia kuunga mkono utekelezaji kupitia ujio wa majiko yenye teknolojia ya kisasa kwa Watanzania wa kipato cha chini.

Dhumuni ni kupunguza athari za kiafya na kijamii zitokanazo na matumizi ya nishati isiyosafi ya kupikia (kuni na mkaa) ambayo imekuwa ikitumiwa kwa muda mrefu hasa maeneo ya vijijini.

Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati imesema ujio wa majiko hayo yanayotumia teknolojia ya kisasa ya Internet of Things (IoT) unalenga kuweka msingi wa mpito kutoka matumizi ya nishati hizo za jadi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa majiko hayo iliyoandaliwa na Shirika la CEFA kwa kushirikiana na Kampuni ya Clean Cooking Technologies S.R.L. (CCT) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa nishati safi ya kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nilasco Mlawi amesema majiko hayo yatasaidia kupunguza matumizi ya nishati isiyo safi kwa Watanzania.

“Kupitia majiko haya ya umeme yenye teknolojia ya kisasa,  yatatolewa majiko 150,000 hadi ifikapo mwaka 2027 itasaidia kutimiza ndoto ya matumizi ya nishati safi ya asilimia 80 ifikapo 2034.

“Wizara tunaunga mkono CCT na CEFA kwa hiki wanachokifanya kwasababu ukiangalia gharama za vifaa vya nishati safi ni ghali sana hivyo wanapokuja wadau kama hawa na unafuu wa vifaa hivyo sisi tunaunga mkono,” amesema.

Lengo la wadau hawa ni kuwafikia wale watu wa hali ya chini ili wapikie nishati safi ambapo ni jambo la msingi huku Serikali ikitoa ushirikiano.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Saad Zaheer kutoka CCT amesema majiko hayo yatakwenda kuzisaidia kaya zenye kipato cha chini lengo ikiwa ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Ili kuepuka uzalishaji wa hewa chafu ambayo inaharibu hali yetu ya hewa ili familia zenye kipato cha chini zinufaike na mradi huu.  Tutatoa katika kaya 5000, lakini mradi huu utaendelea kwa kiwango kikubwa kulingana na uhitaji,” amesema.

Amesema majiko hayo yanalipiwa kidogo kidogo, kila kaya itakayopata haitashindwa kulipia kutokana na unafuu wake na muda wa malipo.

Rogasian Lukoa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi idara ya uratibu wa sekta za uchumi na uzalishaji, amesema uchechemuzi unaofanyika wa kubadilisha mtazamo kwanza wa matumizi ya nishati chafu unasaidia katika kuhamia nishati safi.

“Moja ya jukumu letu ni uhamasishaji. Ujio wa majiko haya yenye teknolojia ya kisasa ni hatua nzuri kwa wananchi kuongeza hamasa ya kuhama kwenye kuni na mkaa,” amesema.

Tendeni Serenge kutoka Mbagala amesema awali wakati anatumia jiko la mkaa alikuwa anapata shida katika kuwaandalia watoto chakula kutokana na ugumu wa upatikanaji wake.

“Jiko hili la umeme ni nafuu gharama yake unalipia Sh50,000 kisha unamalizia kidogo kidogo Sh35,000 ndani ya miezi mitatu. Umeme kidogo unalitumia kwa muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wake, Stratoni Shayo mkazi wa Dar es Salaam amesema jiko la umeme ni bora akilinganisha na kuni ambazo zina madhara kwa afya ikiwemo macho.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa CEFA nchini Tanzania, Cinzia D’Intino, amesema upishi wa nishati safi si suala la teknolojia pekee bali ushirikiano kwanza.

“Kuanzia na mashauriano ya wadau kunatusaidia kuhakikisha mradi huu unatekelezeka, una tija na unakuwa endelevu, huku ukizingatia vipaumbele na uhalisia wa jamii tunazolenga,” amesema.