Na Mwandishi Wetu, Karatu.
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Regina Qwaray, ameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF) kupitia mradi wa OPEC,ikiwemo wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Laja,wilayani Karatu.
Ametoa pongezi hizo jana wilayani humo alipotembelea Shule hiyo iliyojengwa katika Kijiji cha Laja,Karatu mkoani Arusha ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake mkoani humo.
Amesema ujenzi wa shule hiyo umeleta matokeo mazuri kwa jamii ikiwemo kuondoa adha ya wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutokana na kijiji hicho kutokuwa na shule.
“Wanafunzi wengi walikuwa hawafiki shule,wengi walikuwa watoro lakini kupitia mradi huu ambapo hadi mabweni yamejengwa umesaidia kuondoa changamoto hiyo,”amesema
“Niwapongeze wananchi kwa kujitoa kwenu na kuona thamani ya elimu kwani mmeshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuchangia mradi huu,tutunze mradi huu,”
Pia amewataka wazazi kutambua umuhimu wa kusomesha watoto na kuwa elimu ni hazina kwa vijana na inasaidia kuongeza wasomi na kuongeza kasi ya mabadiliko.
Awali Kaimu Mratibu wa TASAF Wilaya ya Karatu, Athanasi Sarwatt,amesema mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Laja umegharimu zaidi ya Sh.milioni 774.9 ambapo TASAF kupitia OPEC awamu ya nne walitoa Sh.milioni 659.5 huku zaidi ya Sh.milioni 115 zikiwa ni michango ya wananchi ikiwemo mchanga,kokoto,mawe,maji na nguvu kazi.
Amesema mradi huo umesaidia kuondoa utoro kwa wanafunzi kwani awali walikuwa wanasafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita nane kwenda shule na kuwa mpango umesaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni hasa wanaotoka kaya maskini sana.
Amesema shule hiyo ilisajiliwa Novemba 2023 na kuanza rasmi mwaka 2024 kwa kupokea wanafunzi 26 wa kidato cha kwanza na kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 63 ambao ni kidato cha kwanza na pili na wote wanakaa bweni.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF mkoa wa Arusha,Richard Nkini,amesema kwa kipindi cha miaka miwili mkoa huo umepokea zaidi ya Sh 23 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imeleta tija na mabadiliko katika jamii.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Juma Hokororo, ameshukuru TASAF kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali hasa ya elimu na kuwa imesaidia kuinua elimu.
Amesema katika kipindi ambacho Shule zinakaribia kufunguliwa,halmashauri hiyo imeweka mikakati kuhakikisha watoto wote ambao wana umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kuripoti shule pamoja na wale waliofaulu wanaotakiwa kujiunga Kidato cha kwanza.







