Wananchi Ngeleli Iringa walia na kero ya kivuko

Iringa. Wananchi wa Mtaa wa Ngeleli, Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa, wameelezea hofu yao juu ya usalama kutokana na ubovu wa Kivuko cha Taro kinachotumiwa na wakazi kuvuka kwenda mashambani, shule na maeneo ya jirani.

Kivuko cha Taro kimekuwa kiungo muhimu kwa wananchi wa Ngeleli, wakikitumia kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, lakini hali yake ya sasa imeifanya jamii hiyo kuishi kwa tahadhari kila siku.

Wakizungumzia kero hiyo leo Januari 11, 2026 mbele ya Mbunge wa Iringa mjini Fadhili Ngajilo, wananchi hao wamesema kuwa kero hiyo  imedumu kwa muda mrefu sasa na imekuwa ikileta usumbufu mkubwa kipindi cha mvua ambapo kivuko hicho hujaa maji na kuwa hatarishi kwa watumiaji.

Kuhusu kero hiyo Ngajilo ametoa maagizo ya moja kwa moja kwa Mtendaji wa Kata ya Ruaha kuhakikisha ukarabati wa kivuko hicho unakamilika ndani ya siku 14.

“Ninataka kuona wananchi wanatumia kivuko salama na bora ndani ya wiki mbili na Serikali ya awamu ya sita haivumilii kuona wananchi wake wakiteseka,” amesema Ngajilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Ruaha, Musa Mbungu, ameeleza kuwa changamoto hiyo imekuwepo kwa muda mrefu na imekuwa ikiwasumbua wakazi, hasa wanafunzi na wakulima wanaovuka kwenda mashambani.

“Tunaamini huu ndio wakati wa mwisho wa kuona kivuko hiki kikiwa katika hali ya kusikitisha kwani tumechoka kuona watoto wakihatarisha maisha yao kila siku,” amesema Mbungu.

Mbunge Ngajilo amesisitiza kuwa ofisi yake iko tayari kutoa usaidizi wowote unaohitajika ili kuhakikisha usalama wa wananchi unasimamiwa ipasavyo.

Pia, ameahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo ili kuona wananchi wanapata nafuu haraka.

Wakazi wa eneo hilo wana matumaini kuwa baada ya hatua hiyo, wataweza kuvuka kwa usalama na kuendelea na shughuli zao bila hofu ya ajali au majeraha.

Hata hivyo, amesema ziara zake katika maeneo ya kata mbalimbali zitaendelea ili kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja na kuzitafutia suluhu kwa ushirikiano wa viongozi wa ngazi zote.