Malkia asimulia Waluguru walivyotumia mawe kujilinda

Morogoro. Waluguru ni miongoni mwa makabila yaliyothamini amani, utulivu na mshikamano lakini walipokabiliwa na maadui hawakusita kujilinda kwa mbinu za jadi ikiwemo adui king’ang’anizi kumporomoshea mawe.

Akizungumza na mwananchi leo Januari 11. 2026 katika tambiko la jadi mjini hapa,  Malkia wa akina mama wa kabila la Waluguru, Wamingila Shilingimbili amesema wazee wao walikuwa wakikimbilia juu ya milima na endapo adui angeendelea kuwafuata walimporomoshea mawe, silaha iliyotosha kumdhoofisha au kumfanya akimbie.

Shilingimbili amesema mbinu hiyo ilikuwa sehemu ya hekima ya kuilinda jamii bila kuvunja mshikamano wao. “Wazee wetu walikuwa na mbinu za kujilinda dhidi ya maadui mbalimbali kuwaporomoshea mawe maadui waliokuwa na ugomvi.”

Shilingimbili amesema wakati huo na sasa wamekuwa wakifanya tambiko la jadi la kuombea taifa amani na utulivu katika jamii chini ya mti wa mtamba kwa kuhusisha wazee wa mila, machifu, wandewa, familia za koo za Waluguru pamoja na viongozi wa serikali ambapo kabla ya tambiko hilo, hufanyika usafi wa mazingira katika makaburi ya waasisi wa mji wa Manispaa ya Morogoro.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Maulid Hassan Dotto (aliyevaa saa waliosimama) na viongozi wengine wa serikali na mila wakiwa katika tambiko la kimila kabila la waluguru la kuombea taifa amani na utulivu katika jamii. Picha na Juma Mtanda.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Shirika la Wazee wa Mila na Desturi Morogoro (Shiwamila), Ramadhan Divunyagale amesema jamii imesahau nguvu na thamani ya mila hali inayosababisha baadhi yao kudharau mambo ya msingi ikiwemo heshima kwa makaburi.

Divunyagale amekemea vitendo vya kutupa taka na kujenga vyoo karibu na makaburi akieleza kuwa si ustaarabu wala utamaduni wa Mwafrika kitendo vinavyopaswa kupingwa kuanzia ngazi ya serikali za mitaa.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Khalid Matengo, amesema tambiko hilo limefanywa kwa wakati muafaka huku akisisitiza umuhimu wa watoto kushirikishwa ili warithi utamaduni na historia ya jamii yao kwani jamii isiyo na historia haina mwelekeo.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Hassan Dotto amesema kuwakumbuka wahenga kwa dua ni nguzo ya amani na maendeleo ya Taifa na kuahidi ushirikiano wa Serikali katika kulinda mila, tamaduni na historia ya Morogoro.

Chifu Lukwele wa nne (Mdimang’ombe) amesema babu yao Chifu Salim Lukwele licha ya kuongoza kabila la Waluguru alikuwa pia akiongoza jamii nyingine.

Mdimang’ombe amesema kabla ya kuanzishwa mji wa Morogoro babu yao na wasaidizi wake walikuwa wakiishi milimani na katika eneo la tambarare kulikuwa na makazi madogo madogo na katika mti wa mtamba ndio ulikuwa eneo maalumu la kufanyia vikao vya machifu.