Wananchi Zanzibar watakiwa kupisha miradi ya maendeleo

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma amesema kila mwananchi atakayepisha ujenzi wa miradi atalipwa fidia na Serikali ya Mapinduzi bila kudhulumiwa.

Hivyo, amewasihi wananchi kuendelea kuiamini Serikali kwa kutoa ushirikiano wa kupisha miradi ya maendeleo inayoendelea kisiwani hapa.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Januari 11, 2026 katika hafla ya ufunguzi wa Barabara ya Kizimkazi ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar.

Hivi karibuni, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliunda tume yenye watu wanane ikiongozwa na Salum Othman Simba ya kupitia na kutathimini masuala ya fidia ikijumuisha wataalamu kutoka taasisi za Serikali na binafsi watakaofanya kazi hiyo.

Hatua hiyo inatokana na utekelezaji wa miradi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Akizungumza katika ufunguzi wa barabara hiyo, Waziri Hamza ameendelea kuwatoa hofu wananchi wapishe miradi kwani Serikali haina nia ya kuwadhulumu.

“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kupisha miradi ya maendeleo  kila mwananchi atakayepitiwa na ujenzi atalipwa fidia bila ya kudhulumiwa fedha zao,” amesema 

Hata hivyo, amewataka wananchi watunze miundombinu inayojengwa na Serikali ili wafaidike nayo.

Amesema Serikali inaandaa vijana wa kuilinda nchi, ndio sababu ya kuunda makundi ya hamasa ya vijana na Serikali inawategemea vijana wake kuwa nchi haiwezi kupinduliwa na mtu yeyote.

Mbali na hilo, amesema sababu ya viongozi kufanya mapinduzi hayo ni madhila na manyanyaso yaliyowanyima haki za msingi ikiwemo kumiliki mali zao binafsi.

Amesema, wakati wa ukoloni wazee waliokuwepo hawakuwa na uwezo wa kufanya chochote ingawaje waliungana kudai uhuru wao bila ya mafanikio yoyote.

Ameeleza kuwa, awali uhuru wa Zanzibar hawakupewa wananchi pekee, alipewa kibaraka wa kisultani kuchukua uhuru huo, hivyo Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume alitafuta wananchi wengine kwa lengo la kuondosha utawala wa kisultani.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Barabara (Zanroads), Safia Juma amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 6.59 imejengwa na Kampuni ya Ecocity Building Materials kwa gharama za Sh8.1 billioni.

Amesema, barabara hizo zitakuwa na upana mita nane na mabomba 44 ya kupitishia huduma za kijamii ikiwamo maji safi na mawasiliano ili kuepuka ukataji wa barabara baada ya kukamilika ujenzi.

Diwani wa Muyuni, Mustafa Mohamed amesema barabara hizo ni fursa na maendeleo makubwa ya mkoa huo kwani awali hawakuwa nazo hivyo wanaahidi kuitunza ili iwanufaishe.