SIKU chache baada ya kuaga Yanga, mshambuliaji Andy Boyeli ameitakia kila la kheri timu hiyo katika mapambano ya kutetea mataji na kusaka ubingwa wa Afrika, huku akimtaja straika Mzimbabwe, Prince Dube.
Boyeli aliyejiunga na Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja mwanzoni mwa msimu huu akitokea Sekhukhune United ya Afrika Kusini, ameitumikia timu hiyo kwa miezi sita na kuifungia mabao mawili kabla ya mabosi wa klabu hiyo ya Jangwani kuamua kusitisha mkataba na kurejesha Sauzi na tayari ameshaaga wiki iliyopita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Boyeli amesema alikuwa na miezi sita bora nje ya uwanja, lakini ndani ilikuwa ni changamoto kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza ila anafurahia kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwa muda mfupi ameonyeshwa upendo mkubwa.
“Sijapata nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini nimeonyeshwa upendo mkubwa kuanzia viongozi wachezaji na hata mashabiki wa Yanga wana upendo mkubwa mno wataendelea kuishi moyoni mwangu,” amesema Boyeli na kuongeza;
“Licha ya changamoto ya kushindwa kufanya kile walichokuwa wanatarajia kutoka kwangu hawakuwahi kuniacha, walikuwa pamoja nami walinipa imani na nguvu ya kupambana zaidi ni furaha kufanya kazi nao.”
Akimzungumzia Dube, amesema ni mshambuliaji mzuri mpambanaji ambaye hakukubali kushindwa na presha ya mashabiki na ukubwa wa timu ndio kitu kinamtoa mchezoni, lakini anaamini akivizoea hivyo atafanya kazi kubwa na nzuri ndani ya timu kwani tayari ameshaaminiwa.
“Dube ni mchezaji mwenye nidhamu kubwa ya mpira, anapenda kazi yake anaangushwa na presha ya ukubwa wa timu ambayo ina mashabiki wanaopenda matokeo mazuri muda wote na yeye bado hajazoea hiyo hali ndio kitu kinamnyima uhuru anajikuta anaingia kwenye mfumo akizoea na kutulia atakuwa bora zaidi ya alivyo sasa,” amesema Boyeli na kuongeza;
“Ni mchezaji ambaye anajituma sana kuanzia uwanja wa mazoezi na kwenye mechi lakini anashindwa kuendana na presha anacheza kwa uoga na kuyavaa yale mashabiki wanayataka ili awe bora anatakiwa kufanya kazi yake bila kuangalia watu watasema nini wakati huo.”
Boyeli amesema Yanga ni timu kubwa ina wachezaji wengi bora wenye uwezo wa kuifikisha mbali timu hiyo wanatakiwa kuaminiwa na kupewa nafasi ili kila mmoja atoe alichonacho bila kukalili nani anafaa kwa wakati huo.
“Yanga ina vijana wenye uwezo mkubwa na wanaipenda timu wapewe nafasi naiona ikifanya vizuri ndani na hata kimataifa uongozi unafanya kazi yao vizuri unaipambania timu benchi pia linamajukumu mazuri litoe nafasi kwa wachezaji ili waonyeshe.”
