KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Konya Amputee inayoshiriki Ligi ya Walemavu nchini Uturuki, Ramadhan Chomelo amesema sababu ya kutoonekana uwanjani ni kutokana na kuchelewa kupata kibali cha kazi.
Kiungo huyo aliachana na Konya msimu uliopita baada ya kuitumikia kwa misimu mitatu mfululizo na tayari amepewa mkataba wa mwaka mmoja na Despas Enerji ya nchini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo amesema kuchelewa kwa kibali hicho kumemfanya akose kucheza mechi sita za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Aliongeza kuwa hadi mwishoni mwa mwezi Januari mambo yatakuwa sawa na amejiandaa vyema kuanza maisha mapya ya ligi hiyo akiwa na timu mpya.
“Kuna changamoto kidogo ya mambo ya kibali cha kazi, lakini naamini kila kitu kitakwenda sawa muda si mrefu,” amesema Chomelo na kuongeza:
“Ni kipindi kigumu kwa mchezaji kukaa nje bila kucheza, lakini nimechukua kama somo la uvumilivu. Nimeendelea kufanya mazoezi kwa bidii ili siku nitakapopata kibali nianze kwa kasi na kuisaidia timu yangu.”
Kiungo huyo amesema kujiunga na klabu mpya ni changamoto nyingine kwake, lakini anaiona kama fursa ya kuanza ukurasa mpya baada ya mafanikio aliyoyapata akiwa Konya Amputee, ambako aliweka rekodi nzuri.
Msimu wake wa kwanza (2022/23) alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na asisti 16, msimu wa 2023/24 alicheza mechi 21 na kufunga mabao manne na asisti tisa na msimu jana aliweka kambani mabao matano na asisti 11.
