Miaka 62 ya Mapinduzi na namna Zanzibar inavyokuza sekta zake kimaendeleo 

Unguja. Wakati leo ikiadhimishwa miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, mabadiliko mengi ya kiuchumi na kijamii yanatajwa kufikiwa ikiwamo maendeleo na haiba ya visiwa hivyo.

Katika kuthibitisha hilo, katika maadhimisho ya mwaka huu jumla ya miradi 107 katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, masoko na nyumba za biashara, makazi na wafanyakazi imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi Unguja na Pemba.

Katika shughuli hizo ambazo zilianza Desemba 22, 2025  na kuhitimishwa Januari 11,2026 miongoni mwa viongozi waliohudhuria ufunguzi wa miradi  hiyo wameelezwa mengi namna mapinduzi yalivyoenziwa.

Akizungumza katika moja hafla ya kuzindua mradi wa shule Kizimkazi, Makamu wa Rais, Dk Emanuel Nchimbi alisema ili kuendeleza mapinduzi yaliyotokea, anashauri kuwapo na umoja na mshikamano kujenga nguvu ya pamoja.

“Wosia wangu mkubwa kwa watu wote, vijana na wazee kwanza umoja wetu uwe na nguvu zaidi tuijue serikali yetu, tuombee dua mambo yote yanayofanyika tufanikiwe na tuzidi kufanikiwa kama ilivyotokea Mapinduzi,” alisema

“Ukiangalia haya yote yanayofanyika ni kutimiza ndoto ya waasisi wa mapinduzi Zanzibar ambayo lengo lake ilikuwa ni kuleta huduma bora kwa wananchi,”alisema Dk Nchimbi

Alisema kabla ya Mapinduzi maisha ya Wazanzibari yalikuwa duni na fursa za masomo zilikuwa chache kwani shule zilikuwa 68 na waliopata nafasi za kusoma walikuwa 25,000 tena kwa ubaguzi mkubwa.

“Sasa ukiangalia katika miaka 62 yamefanyika mabadiliko makubwa kama walivyotarajia waasisi wetu, zimefikia shule 1,200 kutoka 68 zilizokuwapo awali,” alisema.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa sasa kuna wanafunzi zaidi ya 600,000, wakati wa Mapinduzi hakukuwa na chuo kikuu hata kimoja, lakini leo Zanzibar kuna vyuo vikuu vitano.

Kwa upande wa uwekezaji kwa mujibu wa Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, zaidi ya miradi 558 imesajiliwa ikiwa na thamani ya Dola za Marekani 6.9 bilioni ambazo zitatoa ajira 25,000.

Kadhalika Serikali imeweka mikakati ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, na kuunda mazingira rafiki ya biashara na kuifanya sekta ya utalii kuwa moja ya vivutio vya utalii barani Afrika.

Wataalamu wanazungumzia mabadiliko hayo wakisema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii, huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa asilimia 14, kutoka 568,312 Novemba 2023 hadi kufikia watalii zaidi ya 750,000.

Pia, uchumi wa Zanzibar umeonyesha kukua ukifikia asilimia 7.5 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 5.1 mwaka 2021.

Katika sekta uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakar  Hamad, uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia 107.2, kutoka tani 38,107 mwaka 2020 hadi tani 78,943 mwaka 2024.

Bandari na biashara za usafiri wa majini pia ni miongoni mwa sekta ambazo zimeonesha kukua ambapo ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na utanuzi wa bandari za Mkoani na Shumba unatarajiwa kuimarisha sekta ya usafiri wa majini.

Mabadiliko haya yamewezekana kutokana na juhudi za serikali ya Zanzibar katika kuboresha miundombinu, kukuza sekta ya utalii, na kuimarisha uchumi wa buluu.

Wakizungumza kuhusu Zanzibar ilipotoka na ilipo sasa, wananchi na wataalamu mbalimbali wameeleza namna ambavyo kuna mabadiliko makubwa kwenye nyanja za kijamii na uchumi wa nchi.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii Zanzibar, Khamis Ameir Ali alisema kuna mabadiliko makubwa yanayoonekana, hii ni kutokana na kujizatiti katika uimarishaji huduma.

“Katika historia inaelezwa wazi namna ambavyo maisha ya wananchi yalivyokuwa kabla ya mapinduzi, ubaguzi na unyanyasaji wa kikabila na rangi, lakini leo hii tunaona hatua mbalimbali zinazopigwa katika sekta muhimu za huduma,” alisema

“Ukiangalia katika sekta za huduma kama elimu na afya, wakati ule zilikuwa shida na za kibaguzi, waliopata huduma hizo walikuwa wachache hususani wanaotoka katika upande wa watawala.”

Hata hivyo, amesema licha ya hatua hizo bado zinahitajika jitihada za makusudi kuhakikisha hata zile changamoto ambazo bado zinaonekana, ziishe kabisa.

Zulima Haji Amour ni mkazi wa Kiembesamaki Unguja, alisema katika mazingira ya Zanzibar iliyokuwa nayo, hawakuwahi kufikiria kuona mabadiliko makubwa kwa namna inavyoshuhudia sasa.

Hata hivyo, alisema hatua hiyo inatokana na mipango ya serikali kwa kila awamu jinsi viongozi wake walivyokuwa wakutaka kufikia ndoto za waasisi wa Mapinduzi.

“Tunaona mabadiliko mengi ya kiuchumi na kijamii, Zanzibar ya miaka ile sio ya sasa, ikitokea mtu aliyeondoka kipindi hicho akija atapotea, nadhani haya ndio yalilengwa kufanyika kuwakomboa wananchi na kufurahia maisha ndani ya nchi yao,” alisema.

Rais Hussein Mwinyi alitoa msamaha kwa wafungwa 17 waliokuwa wakitumikia adhabu zao magerezani. Kati ya hao 11 wanatokea Unguja na sita ni wa Pemba.