KAMA haitatokea dharura basi tambua kwamba Yanga imefunga rasmi usajili kupitia dirisha hili dogo ikiingiza mashine tano ikigusa idara zote kasoro eneo la makipa tu, huku taarifa tamu kwa mashabiki wa klabu hiyo ni nyota mpya kutoka Uganda, Allan Okello anayetarajiwa kuiwahi fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Yanga imefunga hesabu ikiingiza viungo Mohamed Damaro (Singida Black Stars), Allan Okello (Vipers) ambaye Mwanaspoti linafahamu atatua leo Zanzibar moja kwa moja akitokea kwao Uganda.
Yanga itamtambulisha Okello wakati wowote kutoka leo baada ya kumaliza kuchukuliwa video za utambulisho tayari kwa kuanza kazi kwenye kituo kipya nchini.
Okello atakuwa jukwaani wakati Yanga itakapokuwa inacheza fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kule Pemba kwenye Uwanja wa Gombani itakapopambana na Azam FC.
Mbali na viungo hao Yanga pia inamrudisha beki wa kulia, Yao Kouassi baada ya beki huyo kupona sawasawa goti lake akiwa pia ameshaanza kucheza mechi za kujirudisha katika ubora wake.
Yanga bado inaamini kwenye ubora wa Yao maarufu kwa jina la jeshi, ambapo licha ya kukaa nje kwa takribani msimu mzima, sasa atarudishwa kwenye mfumo wa usajili.
Kule mbele Yanga ilishamuongeza mshambuliaji Emmanuel Mwanengo akitokea TRA United ambapo pia anasubiriwa staa mwingine Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambaye zinamaliziwa taratibu za mwisho kabla ya kuja nchini akitokea Radomial Radom ya Poland.
Ujio wa mastaa hao wapya Yanga itaacha watu na sasa uhakika Denis Nkane alishatolewa kwa mkopo akitua TRA United ambapo pia mshambuliaji Andy Boyeli amrudishwa klabu yake ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini.
Yanga pia inawaondoa Mamadou Doumbia na Moussa Bala Conte ambao kikao na Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said wamekubali kutoka kwa mkopo wakitarajiwa kutua Singida Black Stars.
Awali wawili hao walionyesha kutokubali hatua hiyo, lakini Mwanaspoti linafahamu kulifanyika vikao vizito vya kuweka sawa kila kitu na hatimaye wakakubali kuondoka, huku ikielezwa bayana kwamba dili la kiungo raia wa Togo, Marouf Tchakei limekwama licha ya kuitumikia katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Inaelezwa kuwam, Tchakei anarejea katika klabu yake ya Singida Black Stars kutokana na hesabu za mabosi wa Jangwani kumbeba kiungo mshambuliaji huyo kugoma dakika za mwishoni.
