Steve Barker atoa maagizo mazito Simba

BAADA ya kukaa na kikosi kwa takribani siku kumi na kucheza mechi tatu za Kombe la Mapinduzi 2026, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker ametoa maagizo mazito kwa uongozi katika ishu nzima ya kuboresha kikosi kinachojiandaa kwa mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi y Mabingwa Afrika.

Barker alitambulishwa na Simba Desemba 19, 2025 akichukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyesitishiwa mkataba Desemba 2, 2025 na alianza kazi ya kuinoa timu hiyo Desemba 30, 2025 kabla ya Januari Mosi kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayofikia tamati kesho Junanne.

Inadaiwa kucha huyo ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuharakisha kumletea mashine nne za maana ili kumrahisishia kazi kabloa ya kuanza ngwe nyingine ya mashindano ikiwamo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimesema katika maagizo ya Barker, anataka aletewe mtu eneo la langoni, beki wa kati, kiungo mchezeshaji na mshambuliaji wa pili yaongezewe watu kwani yana changamoto kubwa.

MAAGI 01

“Hayo maeneo ameona yanahitaji maboresho, hivyo ameagiza kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo wasajiliwe wachezaji katika maeneo hayo na uongozi unafanyia kazi,” kimesema chanzo hicho.

Katika eneo la langoni, Simba ina changamoto ya makipa wawili chaguo la kwanza, Moussa Camara na Yakoub Suleiman kupata majeraha wakitarajiwa kurejea Februari mwaka huu, hivyo amebaki Hussein Abel ambaye alicheza mechi mbili za Kombe la Mapinduzi 2026 kati ya tatu, zikiwa ndio pekee alizocheza msimu huu katika mashindano yote.

Beki wa kati, wapo Rushin De Reuck na Chamou Karaboue wanacheza kikosi cha kwanza, huku Abdulrazack Hamza akiwa majeruhi na Vedastus Masinde akiwa bado hajapata muda mwingi wa kucheza tangu atua msimu huu, huku Wilson Nangu alikuwa na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichoshiriki fainali za AFCON 2025. Masinde amecheza mechi za Kombe la Mapinduzi pekee.

MAAGI 02

Januari 8, 2026 wakati Simba ikifungwa 1-0 na Azam FC kisha ikatolewa nusu fainali katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Barker alitaja matatizo yaliyopo kikosini, ikiwamo safu ya ulinzi kushindwa kujilinda kwa mashambulizi ya mipira ya kutengwa na eneo la ushambuliaji kushindwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao sambamba na kutokuwa na ubora wa kuvunja ngome ya wapinzani.

Akizungumzia maboresho ya kikosi hicho, Barker amesema: “Nadhani ni muhimu kutambua kwamba, kama unavyojua, makipa wetu wawili wa chaguo la kwanza kwa sasa ni majeruhi. Hilo ni eneo tunalopaswa kulitazama kwa umakini. Ni jambo la kutia wasiwasi, kwa hiyo ni muhimu tutafute suluhisho.

“Pia kuna maeneo kadhaa ambayo nahisi tunahitaji kuwa bora zaidi na kuimarisha kikosi chetu, hilo tunaamini.  “Lakini tena, kama nilivyosema awali, jambo la muhimu zaidi ni kuikusanya timu, kuleta kundi pamoja. Tunahitaji kuanza kazi. Unajua, katika kushindwa ndipo unapojifunza. 

MAAGI 03

“Hivi sasa tunahitaji kushinda mechi yetu inayofuata ya ugenini kwa ajili yetu wenyewe. Sasa hii ni fursa ya kweli kurejea mazoezini na kufanyia kazi mambo fulani ambayo nahisi lazima tuyafanye kwa ubora zaidi kuliko tulivyofanya awali.”

Simba kwa sasa inajiandaa na mechi ya Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Esperance itakayochezwa Januari 24, 2026 nchini Tunisia, kisha itarudiana nayo wiki moja mbele.

Barker anataka ushindi katika mechi hiyo kutokana na nafasi iliyopo Simba kundini ikiburuza mkia bila pointi kufuatia kupoteza mechi mbili za awali kwa kufungwa bao 1-0 na Petro Atletico ya Angola kisha kufungwa 2-1 na Stade Malien ya Mali.