BAADA ya Yanga kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa winga wa Vipers na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, Allan Okello timu hiyo kwa sasa imevunja rekodi ya usajili ya kikosi hicho na kuivuka iliyokuwa inashikiliwa na Cesar Lobi Manzoki.
Okello amekamilisha usajili huo baada ya mazungumzo ya pande mbili kati ya Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na Lawrence Mulindwa wa Vipers, ambapo wawili hao walikutana tangu wiki iliyopita jijini Kampala Uganda ili kukamilisha dili hilo.
Baada ya dili hilo kukamilika, Yanga imetoa kiasi cha Sh740 milioni ambazo ni $300,000 sawa na UGX1 bilioni za Uganda, akiwa ni nyota wa pili ghali kuuzwa na Vipers, baada ya kiungo mshambuliaji, Farouk Miya aliyejiunga na Standard Liege.
Miya aliyejiunga na Standard Liege ya Ubelgiji mwaka 2016, ndiye mchezaji ghali zaidi kuuzwa na Vipers, ambapo kiungo huyo mshambuliaji aliuzwa kwa Sh986 milioni, ikiwa ni $400,000 ambazo kwa fedha za Uganda ni sawa na UGX1.4 billion.
Nyota mwingine anayefuatia kwa kuuzwa fedha nyingi ni mshambuliaji, Cesar Manzoki aliyeuzwa China mwaka 2022 na kujiunga na kikosi cha Dalian Professional, ambapo Vipers iliingiza Sh493 milioni, ambazo ni $200,000, sawa na UGX721 milioni.
Kwa maana hiyo, Farouk Miya ndiye mchezaji anayeendelea kushikilia rekodi ya kuuzwa kwa kiasi kikubwa cha fedha akitoka Vipers, akifuatiwa na Okello aliyejiunga na Yanga na kumpiku pia, Manzoki aliyekuwa akihusishwa na Simba mara kwa mara.
Okello aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo za KCCA ya Uganda na Paradou AC ya Algeria, anaungana na nyota wengine pia wapya waliosajiliwa dirisha hili dogo, baada ya kiungo, Mohamed Damaro aliyetokea katika kikosi cha Singida Black Stars.
Wengine ni, Emmanuel Mwanengo aliyekuwa TRA United zamani Tabora United na mshambuliaji, Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ raia wa Angola, anayetua ndani ya kikosi hicho akitokea Radomiak Radom ya Poland, ili kwenda kuongeza nguvu mpya.
