Zanzibar. Katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar za kuifanya kuwa kitovu cha kikanda cha usafiri wa baharini na utalii, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeanza kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi (Mpiga Duru).
Mradi huo wa kisasa unakadiriwa kugharimu takribani dola za Marekani milioni 400 (zaidi ya Sh990 bilioni) na unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta za utalii, biashara na usafirishaji, kwa kuhudumia vivuko vya kawaida vya abiria, vivuko vya kasi, meli za Roll-on/Roll-off pamoja na teksi za baharini.
Mbali na hivyo, kituo hicho kitakuwa na eneo la bidhaa zisizotozwa ushuru (duty-free), maduka ya rejareja, marina pamoja na kituo cha ndege za baharini (seaplane), hatua itakayoiimarisha zaidi Zanzibar kama kitovu cha kikanda cha usafiri wa baharini na utalii.
Jana Januari 11, 2026, akisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar, Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Wadogo na Wakubwa wa NBC, Elibariki Masuke, alishiriki katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho, hafla iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.
Amesema Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi kinajengwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), unaohusisha Shirika la Bandari Zanzibar na Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited.
Amesema mradi huo unalenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi na kuboresha ufanisi wa usafiri wa abiria, ambapo unatarajiwa kuhudumia takribani abiria 8,000 kwa siku, sawa na karibu abiria milioni tatu kwa mwaka.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Masuke alisema NBC inajivunia kuwa benki ya kwanza kutoa msaada wa kifedha kwa mradi huo, ikiwemo ufadhili wa mpito (bridge financing) uliotolewa Februari 2024 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza A.
“Mbali na kufadhili ujenzi, NBC itaunga mkono uendeshaji wa kituo hiki kupitia mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji wa mapato katika vituo vya Maruhubi na Malindi, hatua itakayoongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji,” amesema.
Ameongeza ushirikiano kati ya NBC na Zanzibar Ferry Development Company ulianza rasmi mwaka 2024, kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya kampuni hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2023, yenye lengo la kuendeleza vituo vya kisasa vya abiria na mizigo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Zanzibar Ferry Development Company Limited, Jaffer Machano, aliipongeza NBC kwa mchango wake mkubwa katika utekelezaji wa mradi huo.
“Tunaishukuru sana Benki ya NBC kwa ufadhili wake na ushirikiano wa kimkakati. Msaada wa mapema na uendelevu wa NBC umeusogeza kwa kiasi kikubwa mradi huu mbele, na tunatarajia ushirikiano wa muda mrefu utakaochangia kukuza uchumi wa Zanzibar,” alisema Machano.
Alisema NBC pia ilikuwa mwezeshaji mkuu na meneja wa mkopo wa dola za Marekani milioni 200 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, unaolenga kufadhili miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi.
Amesema, benki hiyo inaendesha matawi mawili Zanzibar pamoja na zaidi ya mawakala wa kibenki 200, huku ikiendelea kupanua huduma zake za kifedha kwa lengo la kuunga mkono maendeleo jumuishi ya uchumi wa visiwa hivyo.