Biashara ya viungo vya sehemu za siri inavyochochea ukeketaji – 1

Musoma. Uwepo wa biashara ya siri ya viungo vya binadamu vinavyotokana na ukeketaji umeongeza ugumu wa kutokomeza mila hiyo potofu nchini Tanzania, licha ya kuwapo sera, sheria na kanuni zinazoipiga marufuku.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Wilaya za Butiama, Tarime na Serengeti, mkoani Mara, umebaini imani za kishirikina ndizo huchochea biashara ya siri inayohusisha uuzaji wa sehemu nyeti za wanawake zilizokatwa.

Wakati wa uchunguzi, gazeti hili lilifuata taratibu zote zinazotakiwa na lingeweza kununua sehemu hizo za siri iwapo lingetaka kufanya hivyo, lakini lilisitisha muamala baada ya kuthibitisha kuwa biashara hiyo haramu ilikuwa ikiendelea.

Katika ufuatiliaji huo, imebainika kuwa viongozi wa kimila na ngariba ndio wanaodaiwa kufanya biashara hiyo, ikiaminiwa kuwa wamiliki wa boti za uvuvi huvitumia katika uvuvi na huwalinda dhidi ya mikosi.

Kuendelea kwa ukeketaji katika eneo hilo kumehusishwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi dhaifu na utekelezaji hafifu wa Kifungu cha 118 cha Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 ya mwaka 2019, pamoja na vifungu vya 21, 22 na 169A vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Ni kutokana na hayo, inaelezwa kuwa matukio ya ukeketaji yameongezeka, hali inayohatarisha maisha ya wasichana, ikiwamo kuwaacha na majeraha, msongo wa mawazo na, katika baadhi ya matukio, vifo hutokea.

Kifungu cha 118 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2019 kinakataza waziwazi unyonyaji wa watoto kwa madhumuni yoyote, ikiwamo biashara haramu ya viungo vya sehemu za miili yao.

Wakati huohuo, Kifungu cha 169A cha Kanuni ya Adhabu, marejeo ya mwaka 2022, kinatambua ukeketaji kuwa kosa la jinai.

Vilevile, vifungu vya 21 na 22 vya Kanuni ya Adhabu vinaeleza bayana kuwa kunyamaza, kushindwa kutoa taarifa au kupuuza kuchukua hatua dhidi ya makosa hayo kunahesabika kuwa ni ushiriki katika uhalifu huo.

Chini ya Sheria za Serikali za Mitaa, Sura ya 287 na 288, mamlaka za serikali za mitaa, maofisa watendaji wa vijiji na viongozi wa mitaa wana wajibu wa kisheria wa kulinda haki za watoto katika maeneo yao, kama ilivyoainishwa katika vifungu vya 142 na 143.

Pia, wanatakiwa kuripoti matukio yoyote ya ukeketaji kwa Jeshi la Polisi au maofisa ustawi wa jamii, huku Kifungu cha 13 cha Sheria ya Mtoto kikizitaka mamlaka kulinda watoto dhidi ya mila hatarishi.

Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa licha ya kuwapo ulinzi huo wa kisheria, utekelezaji wake bado ni changamoto.

Mkoani Mara, hususani katika wilaya za Serengeti, Butiama na Tarime, wasichana chini ya miaka 18 wanaendelea kukabiliwa na tishio la ukeketaji, hali inayochochewa na uwepo wa biashara haramu ya viungo vya siri vinavyotokana na ukeketaji.

Takwimu za Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) wa mwaka 2015/16 zinaonesha kiwango cha ukeketaji miongoni mwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 bado ni kikubwa katika eneo hilo, jambo linaloonesha nguvu ya imani za jadi zilizokita mizizi.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa athari za ukeketaji kwa wasichana chini ya miaka 18 ni kubwa na mara nyingi haziwezi kurekebishwa.

Hizi ni pamoja na maumivu makali, kutokwa damu nyingi, mshtuko na, katika baadhi ya matukio, vifo hutokea.

Matumizi ya vyombo visivyo safi huongeza hatari ya maambukizi ya bakteria, Virusi vya Ukimwi (VVU) na homa ya ini, hasa pale zana zinazotumika katika ukeketaji zinapotumika kwa watu wengi.

Mbali na hayo, uharibifu wa tishu na uvimbe unaosababishwa na ukeketaji unaweza kuzuia mkojo, kusababisha maambukizi sugu na kuleta matatizo ya muda mrefu ya uzazi kwa afya ya mama na mtoto.

Ripoti ya mwaka 2025 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kuhusu ukeketaji nchini Tanzania inaonesha utekelezaji hafifu wa sheria zilizopo unaendelea kudhoofisha juhudi za kitaifa za kutokomeza mila hiyo.

“Utekelezaji unabaki kuwa hafifu kutokana na rasilimali chache na hofu ya kukabiliana na viongozi wa kimila. Matokeo yake, kesi nyingi za ukeketaji haziripotiwi na wahusika mara chache hukabiliwa na adhabu za kisheria,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kuhusu upatikanaji wa huduma za afya, ripoti hiyo inabainisha kuwa waathirika wa ukeketaji mara nyingi hupata madhara ya kimwili na kisaikolojia, ikiwamo msongo wa mawazo, matatizo ya uzazi na changamoto za kiafya za muda mrefu.

Inaelezwa kuwa waathirika wengi hawapati huduma bora za afya na msaada wa kisaikolojia, hasa katika jamii zilizotengwa na zilizo mbali.

Wakati wa uchunguzi wa Mwananchi, baadhi ya wavuvi walieleza kuwa Novemba na Desemba ni kilele cha biashara hiyp ya viungo, kwani ndicho kipindi ambacho ukeketaji hufanyika katika jamii nyingi.

Kwa mujibu wa wavuvi hao, viungo vya siri vinavyopatikana kupitia ukeketaji vinaaminika pia kutumika katika shughuli nyingine za kiuchumi, zikiwamo kilimo, ufugaji, biashara na uchimbaji madini.

“Baadhi ya koo, hususani miongoni mwa jamii za Irege na Wagoreme, hufanya mila hiyo katika kipindi hiki. Baada ya sherehe za kukata, wavuvi huwafuata wakeketaji (ngariba) ili kupata viungo hivyo,” anasema mvuvi aliyezungumza kwa sharti la kutokutajwa jina.

Anasema: “Inaaminika kuweka viungo hivyo kwenye boti za uvuvi huleta bahati na kuhakikisha upatikanaji wa samaki wengi.”

Akieleza jinsi biashara hiyo inavyoendeshwa, mvuvi aliyejitambulisha kwa jina la Migi Migi (si jina lake halisi) anasema wavuvi mara chache hununua viungo hivyo moja kwa moja kutoka kwa wakeketaji.

“Mara nyingi ni wamiliki wa boti, ambao pia ndio wafadhili, wanaowafuata wakeketaji au wazee wa kimila kununua viungo hivyo kwa siri,” anasema.

Migi anasema: “Sisi tunaofanya kazi kwenye boti hatununui wenyewe. Tunapewa tu viungo hivyo na kuelekezwa jinsi ya kuvitumia.”

Anasema viungo hivyo wakati mwingine hutumika kuosha boti za uvuvi ufukweni, kwa imani kuwa kuvichanganya na maji ya kuosha vyombo huvutia samaki wengi.

Mvuvi kutoka jamii ya Wakerewe, ambaye amekuwa akijishughulisha na uvuvi tangu mwaka 1993, anasema viungo vya siri hupatikana kwa urahisi katika maeneo ya Kibui na Kinesi, ambako wakeketaji na wazee wa kimila wengi wanaishi.

“Kwa sasa (Desemba), dagaa na sangara ndiyo samaki wanaopatikana kwa wingi, lakini inaaminika kutumia viungo vya siri hugeuka kuwa kichocheo, kinga na kivutio kinachowawezesha wavuvi kupata samaki wengi zaidi,” anasema.

Mvuvi huyo, ambaye jina lake linahifadhiwa, anaeleza kuwa kumiliki viungo vya siri vya binadamu ni kosa la jinai, jambo linalosababisha usiri na tahadhari kuchukuliwa na wahusika.

Anasema wanawake hawaruhusiwi kununua viungo hivyo, akieleza kuwa biashara hiyo inadhibitiwa na wanaume wanaojishughulisha na uvuvi.

Chanzo kingine kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kilifichua kuwa biashara ya viungo hivyo haipo mkoani Mara pekee, bali pia katika mikoa ya Simiyu na Geita.

“Nilishuhudia hili nilipokuwa Mkoa wa Simiyu. Nilimwona mkeketaji akitoka kwenye sherehe ya kukata akiwa amebeba viungo vya siri kwenye ndoo. Nilipouliza, niliambiwa vinachukuliwa kwa ajili ya kuhifadhiwa na baadaye kuuzwa,” anasema.

“Mila hizi zimekuwapo kwa miaka mingi, tofauti ni kuwa hivi sasa zinafanywa kwa usiri zaidi,” anasema.

Rhobi Samwelly, aliyekeketwa, anasema inawezekana viungo vya siri vinavyopatikana kupitia ukeketaji huuzwa, kwani waathirika hawaelezwi kinachotokea baada ya ukeketaji.

“Nilipokeketwa sikuwahi kuona kiungo changu cha siri, na sijui kilipelekwa wapi. Ninachojua ni kuwa msichana anapokatwa, wazee wa kimila na wakeketaji hugawana fedha zinazolipwa na wazazi,” anasema.

Samwelly, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hope for Girls and Women in Tanzania, shirika lisilo la kiserikali linalosaidia wasichana na wanawake wanaokimbia ukatili, ukiwamo ukeketaji, anasema motisha za kiuchumi zinaweza kuwa chanzo kikuu cha mila hiyo.

“Msichana anapokeketwa, wazazi huamini nafasi ya kuolewa huongezeka na wanatarajia kupokea idadi kubwa ya ng’ombe kama mahari,” anasema.

Anaeleza tafiti za kina na uchunguzi endelevu vinaweza kusaidia kufichua na kuvunja mtandao unaohusika na mila hiyo.

“Novemba 2025 pekee, tuliokoa zaidi ya wasichana 200 dhidi ya ukeketaji. Hata hivyo, wengine wengi tayari walikuwa wamekeketwa. Kufikia mwishoni mwa Desemba 2025, wasichana wengi zaidi walikuwa hatarini,” anasema.

Kwa mujibu wa chanzo kingine, vyombo vya dola vilijikita zaidi katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, hali iliyowaacha wahusika wa ukeketaji pasipo ufuatiliaji mkubwa.

Kauli za viongozi wa Serikali

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Itiryo, wilayani Tarime, Veronica Elias, anasema viongozi wa vijiji wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na wadau kupambana na ukeketaji, akieleza kuwa hana taarifa kuhusu biashara ya viungo vinavyotokana na ukeketaji.

“Nimehudumu katika kijiji hiki kwa zaidi ya miaka 10, sijawahi kukutana na tukio la namna hiyo. Kama biashara hiyo ipo, vyombo vya usalama na mamlaka husika vinapaswa kufanya kazi kwa bidii kuivunja na kuisambaratisha,” anasema.

Elias anakiri kuwa ukeketaji bado ni changamoto kubwa katika eneo hilo kutokana na ushawishi wa wazee wa kimila.

Anasema katika baadhi ya matukio wasichana hukeketwa, kisha kuzungushwa hadharani mitaani mchana kweupe kama sehemu ya taratibu za kimila.

Anaeleza kuwa licha ya ushirikiano uliopo na wadau, umbali wa kijiografia wa baadhi ya maeneo huchelewesha mwitikio wa vyombo vya usalama.

“Serikali inapaswa kuongeza fedha ili kuwezesha mamlaka kusimamia na kushughulikia tatizo hili kwa ufanisi zaidi,” anasema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mara, Charles Ezekiel, alipuuza madai kuwa viungo vya siri vinavyotokana na ukeketaji vinauzwa mkoani humo.

“Hizo ni tetesi. Hatuna taarifa zozote kuhusu biashara ya viungo vya siri. Hata hivyo, polisi, kwa kushirikiana na wataalamu wengine, watachunguza madai hayo ili kubaini ukweli wake,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwapo vitendo vya ukeketaji miongoni mwa baadhi ya jamii za Wakurya, akihusisha suala hilo na imani za kitamaduni zilizodumu kwa muda mrefu.

Anasema baadhi ya familia za wafugaji huamini ukeketaji hupunguza hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake, hasa pale wanaume wanapohama kwa muda mrefu kutafuta kipato kupitia uchimbaji madini au shughuli nyingine.

“Wanaamini kukata wanawake kunahakikisha uaminifu wa ndoa wakati wanaume wanapokuwa mbali. Hicho ndicho kinachoelezwa kuwa chanzo cha mila hiyo,” anasema.

Anapuuza madai yanayohusisha ukeketaji na mafanikio ya uvuvi au uchimbaji madini, akisema hakuna ushahidi unaothibitisha madai hayo.

“Kama matumizi hayo yangekuwapo, yangekuwa yanajulikana muda mrefu uliopita. Hakujawahi kuwa na uthibitisho rasmi wa madai hayo,” anasema.

Sebastian Kitiku, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, anasema wizara haina taarifa ya kuwapo biashara ya viungo vitokanavyo na ukeketaji.

“Hatujui kama viungo hivi vinauzwa, vinauzwa kwa watu gani, au jinsi gani miamala inafanyika. Ikiwa biashara hiyo inafanyika, basi ni kinyume cha sheria kwa sababu ni haramu. Bila shaka itakuwa inafanyika kwa siri sana, kwa sababu kitendo hicho ni kinyume cha sheria,” anasema, na kuongeza:

“Hivi sasa hatuna taarifa rasmi zinazoonyesha bidhaa hizi zinauzwa. Hata hivyo, ikiwa taarifa hiyo ni kweli, ni dhahiri yeyote anayehusika anashiriki katika biashara haramu.”

Anasisitiza kuwa hata kama biashara hiyo ingekuwapo na mtu akanunua viungo hivyo kupitia njia hiyo, bidhaa hiyo haiwezi kumletea mtu utajiri au mafanikio.

“Huu ndiyo ujumbe tunaoendelea kuusisitiza,” anasema.

Anasema ili viungo hivyo viuzwe, ukeketaji lazima uwe umefanyika, akibainisha kuwa kitendo hicho kinapofanyika kinafanikisha biashara hiyo kuwapo.

Kitiku anasema sheria inashughulikia wanaofanya ukeketaji, na kubainisha kuwa inapaswa sasa iwaangukie wanaojihusisha na biashara hiyo.

Anaeleza ushahidi unahitajika katika kuwatambua wanaojihusisha na biashara hiyo ili sheria ichukue mkondo wake.

“Kama kuna ushahidi au taarifa zilizothibitishwa kuwa shughuli hiyo inafanyika, tunawahimiza wote wenye taarifa sahihi juu ya wapi na jinsi matukio hayo yanavyotokea kuziwasilisha kwa mamlaka husika. Hii itawezesha kuwabaini wahalifu na kuwachukulia hatua za kisheria,” anasema.

Ukeketaji umegawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni:

Kuondoa sehemu au kisimi chote, pamoja na mkunjo wa ngozi unaozunguka sehemu ya siri ya mwanamke.

Kuondoa sehemu au kisimi chote na labia ndogo (mikunjo ya ndani ya uke), pamoja na au bila kuondolewa kwa labia kubwa (mikunjo ya nje ya ngozi ya uke).

Kupunguza mwanya wa sehemu ya uke kwa kukata na kuweka upya labia ndogo au kubwa, wakati mwingine kwa kushona na pasipo kuondolewa kisimi.

Taratibu nyingine zenye madhara kwa sehemu ya siri ya mwanamke kwa madhumuni yasiyo ya matibabu, kama kutoboa, kuvuta, kuchanja, kukwarua na kuzichoma.