Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ametoa wito kwa askari wa Jeshi la Polisi na watumishi wote wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu ya hali ya juu, uadilifu na uzalendo, akisema nafasi walizonazo ni dhamana kwa jamii na si miliki binafsi.
Akizungumza Januari 12, 2026 katika hafla ya utoaji wa nishani za heshima kwa askari waliofanya vizuri kwa mwaka 2025 katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Manispaa ya Iringa, RC James amesema kuwa kabla yao kulikuwa na waliowahi kushika nafasi hizo, hivyo ni muhimu kuzitumia kwa manufaa ya wananchi.
Katika hafla hiyo, jumla ya askari 25 walitunukiwa nishani kwa utendaji mzuri, nidhamu na mchango wao katika kuhakikisha usalama wa wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James (aliyevaa suti) akikabidhi nishani ya heshima kwa askari mmoja wapo wa waliofanya vizuri kwa mwaka 2025 katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Manispaa ya Iringa. picha na Christina Thobias
“Nafasi uliyonayo leo si ya kudumu. Kabla yako walikuwepo wengine, na baada yako watakuja wengine na kinachobaki ni alama utakayoacha kupitia utendaji wako,” amesema RC James mbele ya viongozi wa vyombo vya ulinzi, usalama, ndugu na jamaa wa askari waliotunukiwa nishani.
RC James amesisitiza kuwa nidhamu kazini ni msingi wa utendaji bora, hasa kwa askari wa polisi ambao wamepewa jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao.
Askari waliotunukiwa nishani walipongezwa na huku wakihimizwa kuendelea kuwa mfano kwa wengine katika kazi zao.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, SACP Allan Bukumbi akizungumza katika hafla ya utoaji wa nishani za heshima kwa askari waliofanya vizuri. picha na Christina Thobias
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, amesema tuzo zilizotolewa ni sehemu ya kuwatambua askari wanaojituma kwa weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Tunatambua na kuthamini mchango wa kila askari na waliopata tuzo leo wameonyesha mfano mzuri wa nidhamu, uzalendo na kujitoa kwao kwa wananchi hivyo tunatarajia wengine wataiga mfano huu,” amesema Bukumbi.