Tanga. Majeruhi sita kati ya 13 waliokuwa wakipatiwa huduma za matibabu baada ya ajali ya kugongana uso kwa uso kati ya magari mawili, iliyotokea eneo la Mkumbara, Tarafa ya Mombo, wilayani Korogwe, kwenye barabara kuu ya Same–Korogwe, wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo kufuatia hali zao kuwa mbaya.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mombo, John Mapolu, amesema majeruhi wengine 13 waliopata majeraha katika ajali hiyo wameendelea vizuri na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya zao kuimarika.
“Majeruhi waliokuwa na hali mbaya tuliona ni vyema kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo kwa matibabu zaidi. Kesi zilizokuwa za kawaida tulizihudumia hapa, na hadi leo asubuhi Januari 12, tumewaruhusu kurejea nyumbani,” amesema Mapoli.
Kuhusu miili ya marehemu iliyokuwa imehifadhiwa katika kituo hicho cha afya, Dk Mapoli amesema tayari imeshatambuliwa na jamaa zao, huku taratibu za kuichukua kwa ajili ya mazishi zikiendelea.
Ajali hiyo ilitokea Januari 11 saa 9:30 asubuhi, ikihusisha gari la mizigo aina ya Scania mali ya kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Ltd, likiwa limeunganishwa na trela pamoja na basi la abiria aina ya Yutong mali ya kampuni ya Mwensino.
Gari la mizigo lilikuwa likitokea Same kuelekea Korogwe, wakati basi la abiria lilikuwa likitokea wilayani Lushoto kuelekea mkoani Arusha.
Katika ajali hiyo, watu wanne walipoteza maisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Alimachius Mchunguzi, amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo, huku akitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendo kasi, uzembe na maamuzi hatarishi ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.
