Waziri Ndege: Watoto wenye mahitaji maalumu wasifichwe

Babati. Jamii nchini imetakiwa kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye uhitaji maalumu majumbani, kwani kufanya hivyo kunawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu, malezi bora na fursa za maisha.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, Regina Ndege ameeleza hayo leo Januari 12, 2026 wakati akigawa viti mwendo 10 kwa watoto wenye ulemavu kwenye kikao cha Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Babati vijijini mkoani Manyara.

Ndege ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Manyara, ameeleza kuwa  watoto wenye uhitaji maalumu ni sehemu ya jamii na wanapaswa kuonekana, kusikilizwa na kupewa nafasi ya kusoma na kutimiza ndoto zao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Regina Ndege  ambaye pia ni mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, akimbeba mtoto baada ya kukabidhi viti mwendo kwa watoto wenye mahitaji maalum halmashauri ya wilaya ya Babati. Picha na Joseph Lyimo

Ameeleza kwamba wazazi na walezi wasiwe na dhana potofu ya kuwaficha kwani wakipatiwa elimu wanakuja kuwa msaada kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema viti mwendo vilivyokabidhiwa vitasaidia kuwaondolea vikwazo vya usafiri, hasa wakati wa kwenda shuleni, na kuwapa uhuru wa kujitegemea zaidi huku pia vikiwapunguzia mzigo wazazi na walezi.

“Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha mazingira ya elimu jumuishi, ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wa viungo au wa akili wanapata elimu sawa na watoto wengine,” amesema Ndege.

Hata hivyo, Ndege amewataka wazazi na walezi kuhakikisha viti hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na havifanyiwi biashara.

Baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum wa halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini mkoani Manyara, wakiwa na viti mwendo walivyokabidhiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Regina Ndege. Picha na Joseph Lyimo

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Babati vijijini, Agatha Raphael amemshukuru Ndege kwa moyo wake wa kusaidia jamii yenye uhitaji na kutoa viti mwendo hivyo 10.

Theodora Matheo, mzazi wa mtoto mwenye ulemavu ametoa shukurani nyingi kwa Naibu Waziri huyo kwa kuwajali watoto wao.

Amesema hawana cha kumlipa kutokana na msaada huo zaidi ya kumuombea kwa Mungu amzidishie uzima na afya ili aendelee kuwatumikia Watanzania.