Ziara ya Dokta Migiro iliyobeba kauli mbiu isemayo ShinaLakoLinakuita, tayari imeshafanyika katika wilaya ya Temeke, Kigamboni, Ubungo na Kinondoni na kesho itafanyika wilayani Ilala kwa kuzungumza pia na Mabalozi wa mashina katika ukumbi wa Diamond Jublee.
Katika ziara yake Katibu Mkuu wa CCM, anazungumzia zaidi nguvu ya wanachama walioko katika mashina, matawi, huku akisisitiza nafasi ya wazee katika kutoa elimu ya itikadi kwa vijana
Siku ya kwanza ya ziara, akizungumza na mabalozi wa mashina wa Wilaya za Temeke na Kigamboni katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa PTA uliopo Sabasaba jijini Dar es Salaam, Dokta Migiro, alisema kuna kila sababu ya kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinazingatia utaratibu wa kusikiliza maoni na ushauri kuanzia ngazi ya chini badala ya utaratibu wa maelekezo kutoka juu kwenda chini.
Alitumia pia kikao hicho kutoa rai kwa viongozi na wana CCM kuzingatia utaratibu wa kutoa maoni kuanzia ngazi ya chini kwenda juu.
“Nitoe wito kwa viongozi wetu tusifanye utaratibu wa kutoa amri kutoka juu kushuka chini maana uongozi mzuri ni lazima uanzie chini kwenda juu, yale tunayoyapata kutoka kwenye mashina, matawi ndio yatapanda juu kwa lengo la kukiimarisha chama chetu, alisema Dkt.Migiro.
Aidha, siku iliyofuata katika ziara yake, akizungumza na viongozi wa mashina na matawi wa Wilaya za Kinondoni na Ubungo, Katibu Mkuu huyo wa CCM, alisema Chama Cha Mapinduzi hakijengwi katika majukwaa, bali hujengwa kuanzia ngazi ya mashina na matawi, huku akibainisha majukwaa hutumika zaidi kwa ajili ya kutoa hamasa.
“Mashina ndiyo moyo wa CCM kwa kuwa ndiyo yanayokutanisha chama na wananchi moja kwa moja kupitia vikao na shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa, amesisitiza Dk.Migiro, anayeendelea na ziara yake mkolani Dar es salaam yenye kauli mbiu ShinaLakoLinakuita.


