Unguja. Licha ya kutofanyika sherehe za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar, vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vimeadhimisha siku hiyo kwa kufanya matembezi maalumu na mazoezi ya kawaida kuweka mwili katika hali ya utayari.
Majeshi hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Vikosi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), wameahidi kuendelea kushirikiana kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa kama yalivyokuwa malengo ya Mapinduzi.
Matembezi hayo ya kilomita nane yaliyojumuisha majeshi sita, yameanzia Mtoni hadi viwanja vya Mnazimmoja Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja Zanzibar.
Wakizungumza baada ya matembezi hayo leo Jumatatu Januari 12, 2026, wakuu wa majeshi hayo wamesema wataendelea kushirikiana kwa karibu, ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa na wananchi wanafanya shughuli zao bila hofu wala bughudha.
Wamesema mshikamano uliopo baina yao ni nguzo muhimu katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu na changamoto mbalimbali za kiusalama kwa masilahi ya Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Nyuki Zanzibar, Jenerali Said Khamis Said amesema suala la kulinda amani katika nchi halina mbadala kwani ndio inayowezesha wananchi kufanya mambo yao vizuri na kuiwezesha Serikali kuleta maendeleo, ambayo ndio lengo la Mapinduzi kuhakikisha wananchi wanajitawala wenyewe.
Akizungumzia kilele cha Mapinduzi amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimeamua kushirikiana kuadhimisha kipekee kuonesha ukakamavu na utayari katika kulinda amani, raia na mali zao.
Jenerali Said, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Zanzibar, amesema matembezi hayo ni sehemu ya mafunzo ya mara kwa mara kwa askari, yanayolenga kuimarisha uimara wa mwili na akili pamoja na kudumisha nidhamu ya kijeshi.
“Tukio hili limekuwa sehemu ya kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar kwa vitendo, huku likionesha ushirikiano uliopo baina ya vyombo vya ulinzi vya SMT na SMZ katika kutekeleza majukumu yao ya kitaifa,” amesema
Ametumia fursa hiyo pia kuwataka askari hao kushirikiana na kuishi na wananchi vizuri katika maeneo yao.
Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Zanzibar, amesema Januari 12 ni siku muhimu kwa wananchi wa Zanzibar kwani huadhimisha Mapinduzi Matukufu yaliyoleta uhuru, amani na maendeleo.
“Safari hii tumeamua kuadhimisha siku hii adhimu kwa namna ya kipekee kwa kushirikiana kama vyombo vya ulinzi na usalama, tukifanya matembezi ya pamoja kama ishara ya mshikamano wetu,” alisema.
Amebainisha ushirikiano huo unaonesha vyombo vya ulinzi na usalama vipo pamoja katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiserikali, hususan pale inapojitokeza changamoto za kiusalama.
Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama Zanzibar, Kamishna Kombo amesema wanamshukuru Mungu kwani wamehitimisha mwaka uliopita katika hali nzuri, huku matukio ya uhalifu yakipungua na kuanza mwaka mpya kwa matumaini na mikakati mipya ya kuimarisha usalama.
Ameahidi kuwa vyombo hivyo vitaendelea kushirikiana kwa karibu mwaka huu ili kudhibiti changamoto zozote kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa mahali salama kwa wananchi na wageni.
Kamishna Kombo amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa haulipi badala yake huleta madhara kwa mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla hivyo ni lazima kujiweka mbali nao na kuhakikisha wanatekeleza na kufuata sheria za nchi.
“Unapofanya uhalifu ujue tu utakupeleka pabaya na haiwi sifa njema ikiwa unajishughulisha na jambo hilo kama kijana ama mzazi kwani ukienda kinyume, sheria itachukua mkondo wake,” amebainisha.
Azana Hassan Msingiri ni Kamanda Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Zanzibar, amesema matembezi hayo ni ishara ya kuenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kuimarisha mshikamano wa vyombo vya ulinzi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Amesema Mapinduzi ya Zanzibar yameweka msingi imara wa amani na usalama, hivyo viongozi na wananchi wana wajibu wa kuyatetea na kuyahifadhi kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Msingiri ameahidi kuwa wanajeshi wataendelea kuheshimu viapo walivyokula na kulinda Mapinduzi pamoja na usalama wa nchi kwa nguvu na mshikamano wao wote.
“Tutahakikisha visiwa vyetu vinaendelea kuwa salama, wananchi wakitekeleza shughuli zao katika mazingira ya amani na utulivu, kwani amani ndio msingi wa maendeleo ya Taifa letu,”amesema.
Wametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwani ndio msingi wa kudumisha amani ya kudumu nchini.
