Dar es Salaam. Utafiti mpya uliotolewa na Benki ya Dunia (WB) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika sekta ya umma.
Hatua hiyo inataja kuthibitisha mafanikio ya mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kutekelezwa na Serikali.
Kwa mujibu wa Ripoti hiyo ya Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika Utoaji wa Huduma za Serikali na Ushirikishwaji wa Wananchi (GovTech Maturity Index – GTMI) ya Benki ya Dunia mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A, ukomavu wa juu wa matumizi ya Tehama.
Kundi hili linalojumuisha nchi zinazoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Ripoti hiyo hutathmini kiwango cha ukomavu wa Tehama serikalini takriban katika nchi zote duniani, kwa kuzingatia maeneo mbalimbali yakiwamo ya sera, sheria, miongozo, mifumo na utekelezaji wake ambapo katika mwaka uliopita ripoti hiyo ilitolewa Desemba, 2025.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kutambuliwa na Benki ya Dunia katika kupiga hatua ya ukomavu wa Tehama, mwaka 2022 Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi duniani katika GovTech Maturity Index.
Katika utafiti huo uliohusisha nchi 198, Tanzania ilipanda kutoka nafasi ya 90 mwaka 2021 hadi nafasi ya 26 mwaka 2022 na kutoka kundi B hadi kundi A. Barani Afrika, Tanzania ilishika nafasi ya pili baada ya Mauritius na kuwa kinara wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Benedict Ndomba mafanikio hayo ni ushahidi wa mwelekeo sahihi wa Taifa katika kujenga Serikali ya kidijitali.
“Benki ya Dunia imefanya utafiti huu kwa takriban mwaka mmoja huku ikikusanya uthibitisho na taarifa mbalimbali kwenye matumizi ya Tehama Serikalini katika nchi mbalimbali duniani,” amesema.
Amesema uwepo wa mifumo mbalimbali ya Tehama serikalini inaonesha usimamizi mzuri wa rasilimali za Tehama na kutoa wito kwa taasisi za umma kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali mtandao katika utekelezaji wa miradi ya tehama.
“Pia nahimiza matumizi ya mifumo ya ushirikishwaji wa wananchi na kuunganisha mifumo ya taasisi na GovESB,” amesema.
Amesema mafanikio haya yanaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mageuzi ya kidijitali barani Afrika na kuweka msingi imara wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za umma, kukuza uwazi na kuimarisha uchumi wa kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Amesema kuimarika kwa nafasi ya Tanzania Kimataifa ni mwendelezo wa safari ya Tanzania ya kupanda ngazi katika ukomavu wa tehama serikalini na kuendelea kujijengea taswira chanya kimataifa na kikanda.
Kwa upande wa Afrika, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi vinara wa mageuzi ya kidijitali serikalini, ikilinganishwa na mataifa mengine yaliyofanyiwa tathmini katika ripoti hiyo.
Tanzania ni moja kati ya nchi tano tu katika bara la Afrika ambazo zimeingia kwenye kundi la juu la ukomavu wa Tehama Serikalini na nchi nyingine ni Kenya, Misri, Uganda na Rwanda.
Katika ripoti ya mwaka 2025 maeneo manne yaliyoangaziwa ni mifumo ya mikuu ya Serikali, huduma zinazotolewa mtandaoni, jukwaa la ushirikishwaji wananchi kidijitali na mazingira wezeshi.
Ikielezea zaidi mambo yaliyoibeba Tanzania ripoti hii inaonesha kuwa mafanikio ya Tanzania yametokana kwa kiasi kikubwa na uwepo na matumizi ya mifumo ya mikuu ya Serikali.
Mifumo hiyo imejumuisha ile ya usimamizi wa rasilimaliwatu kama vile mfumo wa taarifa za watumishi na Mishahara, mifumo ya ajira (Ajira Portal) na mifumo ya kuunganisha na kubadilishana taarifa kati ya taasisi za umma.
“Pia mfumo mkuu wa ubadilishanaji taarifa serikalini umetajwa kuwa mhimili muhimu unaowezesha mifumo ya taasisi mbalimbali za umma kusomana na kubadilishana taarifa kwa usalama na ufanisi zaidi,” amesema.
Hatua hii imepunguza urudufu wa taarifa, kuharakisha utoaji wa huduma na kuongeza uwajibikaji.
Katika upande wa ushirikishwaji wa wananchi kidijitali, Tanzania imetajwa miongoni mwa nchi zinazochukua hatua madhubuti katika kujenga mifumo inayowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika masuala ya utawala.
Pia, Mfumo wa e-Mrejesho umekuwa ni nyenzo muhimu inayowaunganisha wananchi na Serikali, kwa kuwezesha utoaji wa maoni, malalamiko, ushauri na pongezi, pamoja na kupata mrejesho kwa wakati. Mfumo huu umechangia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi kwa Serikali.
Wakati Benki ya Dunia ikiitambua Tanzania, Mtaalamu wa Teknolojia, Lawrence Msaki ameitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kufanya marejeo ili kujua uimara wa mifumo yake kila wakati ili iwe salama.
“Kutambuliwa ni suala zuri lakini ni lazima tuhakikishe tunajilinda ili isiweze kuingiliwa kirahisi, kila baada ya muda fulani tufanyie mapitio ili iwe imara juu ya mtu yoyote mwenye nia ya kuichezea,” amesema.
