Wananchi waeleza adha siku sita bila kivuko cha Mv Kazi

Dar es Salaam. Wakati Kivuko cha ‘Mv Kazi’ kikiwa kimefikisha siku sita bila kufanya kazi, wananchi wa Kigamboni wameeleza adha wameipata kutokana na hali hiyo.

Wananchi wamesema hayo leo Jumatatu Januari 12, 2026 baada ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Moses Mabamba, kueleza kutarajiwa kuanza tena kazi kwa kivuko hicho kesho Jumanne baada ya matengenezo yake kamilika.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti kuhusu hatua hiyo, Juliana Didas amesema taarifa hizo ni njema kwao ukizingatia baadhi walikuwa hawana uwezo wa kulipia Sh500 kwa vivuko vilivyokuwa vikifanya kazi.

“Kawaida vivuko hivi vya Serikali tunalipa Sh200, hivyo kuna watu bajeti yao ni Sh400 kuvuka kila siku, hivyo kurudi kwa kivuko cha serikali ni jambo la kushukuru “amesema Juliana.

Abiria wakiwa wanashuko katika vivuko ambavyo kesho vitatumika kuwabeba wanafunzi bure

Naye Job Masinyilo, amesema kivuko cha Mv kazi ubovu wake umekuwa mara kwa mara jambo liilokuwa likiwapa wasiwasi watu wanaokipanda.

Hata hivyo, ameshauri kuongezwa kwa kivuko hicho, walau viwe vinapishana kwa kuwa ilikuwa ikiwalazimu kusubiri hadi nusu saa kivuko kifike kutoka upande wa pili na hivyo kuchelewa katika shughuli zao za kujitafutia riziki.

Daud Kisaka, mkazi wa Tungi, amesema kutokana na kuwa na gari humlazimu kupita daraja la Mwalimu Nyerere, kwa kuwa vivuko vinavyofanya kazi havitoi huduma ya kubeba magari.

Hali hii Kisaka amesema inamfanya kupambana na foleni za barababarani jambo linalomlazima kubadilisha saa za kutoka nyumbani lakiki pia kuongeza gharama katika ununjaji wa mafuta ya gari.

“Kupitia Kivuko kulinifanya niamke saa moja na ninawahi vizuri kazini kwa sababu hainichukui hata nusu saa nakuwa nimefika, lakini kwa sababu ya sasa kupita darajani imebidi nisogeze saa nyuma za kuamka lakini pia nachelewa kurudi nyumbani na kukosa muda wa kutosha wa kukaa na familia yangu,” amesema Kisaka.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kurejea kesho kwa kivuko hicho, Mabamba amesema kitaanza kwa majaribio asubuhi ya kesho Januari 12, 2026 kabla ya kubeba abiria, kwa kuwa hilo ni takwa la kisheria chombo kinapotoka kwenye matengenezo.

“Kivuko hiki kiliharibika tangu Januari 6, 2026, ambapo tuliamua kukitengeneza kwa kutengeneza injini zake zilizokuwa zimeharibima na kuongeza nyingine mbili na hivyo kuwa na unjini nne kwa sasa.

“Pia, tulifanya marekebisho katika mifumo yote ya umeme na kiuendeshaji ili kiweze kufanya kazi wakati wote badala ya kilivyokuwa kikifanya kazi na kusimama,” amesema Mabamba.

Hata hivyo, Mabamba amesema kwa kuwa kesho wanafunzi wanafungua shule, wamewaombea kubebwa bure katika vivuko vya kampuni ya Azam.

“Nadhani wote mnajua kuwa kesho shule zinafunguliwa na kwa kuwa kivuko chetu hakijatengemaa tumeomba wenzetu Azam watusaidie kuwabeba wanafunzi ambao katika vivuko vyetu siku zote huvushwa bure bila kuwatiza hela yoyote.

“Katika hili kikubwa mwanafunzi awe katika sare za shule au awe na kitambulisho na katika upandaji watakuwa na foleni yao,”amesema Mabamba.

Pia, ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi waliopata usumbufu katika siku zote hizo ambapo kivuko kilikuwa kwenye matengenezo.

Kivuko cha Mv kazi kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 20 kwa wakati mmoja huku ukarabati wake ikielezwa umetumia siku nne na kugharimu Sh30 milioni.

Abiria wakiwa wanashuko katika vivuko ambavyo kesho vitatumika kuwabeba wanafunzi bure

Kuhusu Mv Magogoni na Mv Kigamboni

Akizungumzia kuhusu kivuko kikubwa kuliko vyote cha Mv Magogoni ambacho kilikuwa katika matengenezo nchini Kenya tangu Februari 2022, Mabamba amesema kinatarajiwa kuwasili nchini Aprili 2026.

“Mpaka ninavyozungumza sasa kivuko hicho matengenezo yake yamefikia asilimia 81.3, hivyo ni matarajio yetu hadi kufika Aprili mwaka huu kitakuwa kimewasili nchini tayari kwa kuanza kutoa huduma.

Kivuko cha Mv Kigamboni kina uwezo wa kubeba abiria 2000 na magari 60 kwa wakati mmoja.

Wakati kivuko cha Mv Kigamboni amesema nacho ifikapo Oktoba 2026, kitakuwa kimerejea kutoka kwenye matengenezo makubwa na hapo ndio kivuko cha Mv Kazi nacho tutakipeleka kwenye matengenezo kama hayo.

Alipoulizwa kama kuna mpango wowote wa kuleta kivuko kipya ukiacha hivyo vilivyopo, Mabamba amesema hakuna mpango huo kwa kuwa wanaamini vivuko vyote vikiwa vizima vina uwezo wa kuwahudumia wananchi bila shida.