ACT-Wazalendo yawapiga msasa wabunge wake

Dar es Salaam. Chama cha ACT–Wazalendo kimewapiga msasa   wabunge wake wapya ili kujiandaa kutekeleza majukumu yao ya kuisimamia Serikali katika Bunge la Tanzania.

Katika Bunge hilo la 13, linalotawaliwa na uwingi wa wabunge wa Chama cha Mapinduzi  (CCM),  ACT–Wazalendo itawakilishwa na wabunge wanane, kati ya wabunge 11 wa Vyama vya upinzani huku wanaobakia wakitoka Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Vikao rasmi vya Bunge hilo, vitaanza Januari 27, 2026, ingawa vikao vya kamati za kudumu vimepangwa kuanza kesho Jumanne na kuendelea hadi Januari 26.

Pamoja na mambo mengine, vikao vitakavyoanza kesho, wabunge watajua kamati zao za kudumu, kuchagua wenyeviti na makamu wao na kuelezwa majukumu yao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma, leo Januari 12, 2026 na Naibu Katibu Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi, Mbarala Maharagande, amesema kiongozi wa chama hicho,  Zitto Kabwe ameshiriki na kutoa mafunzo maalumu (semina) kwa wabunge hao.

“Tumetoa mafunzo kwa wabunge wanaotokana na chama chetu, ACT Wazalendo ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kibunge, kwa ufanisi,” amesema Maharagande.

Maharagande amesema mafunzo hayo yamehudhuriwa na wabunge wote wa chama jijini Dodoma, yakiwa na lengo la kubadilishana uzoefu na namna ya kuisimamia ipasavyo Serikali, kuwawakilisha wananchi na kutunga sheria ikiwa ndio wajibu wa msingi kwa wabunge.

Akizungumza katika mkutano huo, Zitto ameeleza uzoefu wake wa siasa za kibunge katika kuleta ufanisi na matokeo chanya kwa masilahi ya Taifa, ya chama na wananchi (jimboni) kwa Mbunge husika.

Maharagande amesema kutokana na mafunzo hayo wabunge anaamini wapo tayari kutekeleza majukumu yao ya Kibunge na kuiwajibisha Serikali kwa masilahi mapana ya Taifa.

“ACT Wazalendo itaendelea na wajibu wake wa msingi wa kuwasemea na kupigania ustawi mwema wa Taifa letu kwa kuhakikisha nchi yetu inaheshimu na kuwa na utawala wa sheria, demokrasia, na kulinda misingi ya haki za binadamu,” amesema Maharagande